NA MOHAMED HAKIM

WATUMISHI wa umma wametakiwa kutofanya kazi kimezaoweya na badala yake wafanye kazi kwa uzalendo na uwadilifu, kwalengo la kuisadia serikali kutimiza azma ya kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo ya taifa kiujumla.

Ofisa Msaidizi Idara ya Mafunzo mafupi na Kujenga Uwezo, kutoka Chuo cha Utawala wa Umma (IPA) Hassan Juma Issa, aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya watumishi wa umma wapya kutoka taasisi mbalimbali za serikali yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu katika ukumbi wa IPA Jumbi Wilaya ya Kati Unguja.

Alisema, kwa muda mrefu wafanyakazi wa taasisi za serikali wamekuwa wakifanya kazi kimazoe na kutofuata taratibu za kiutumishi katika kutekeleza majukumu waliopangiwa, jambo ambalo linarejesha nyuma juhudi za serikali katika kufikia malengo yake.

Aliongeza kuwa, ili wafanyakazi waweze kufanyakazi kiufanisi lazima wawe na uzalendo na wenye kuyajua maadili ya utumishi wa umma, sifa ambazo watu wengi wanaofanya kazi kwenye taasisi za serikali na binafsi wamezikosa.

“Kama wafanyakazi wa taasisi za umma lazima tuzipende kazi zetu na tuwe wazalendo kwa kufanya kazi kwa bidii, kuhakikisha matarajio ya serikali yanafikiwa, kwani kufanya hivyo kutalisaidia sana taifa letu kusonga mbele” alisema Hassan.

Hivyo aliwataka watumishi hao wapya wa umma, kufuata yale yote waliyoelekezwa kipindi cha mafunzo hayo, ili wakawe mfano bora katika taasisi zao na wenye kuleta mabadiliko na maendeleo ya haraka katika nchi.

Aidha akizungumza baada ya mafunzo hayo mmoja wa washiriki Salma Mohamed Salum kutoka Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), aliushukuru uongozi wa chuo hicho kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewajenga kimaadili na kiuzalenda pamoja na kuwapa moyo wa kulitumikia taifa lao.

Nae Shaban Omar mshiriki kutoka Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, aliiomba taasisi ya IPA kuendelea kutoa mafunzo hayo sio kwa waajiriwa wapya pekee bali hata wakuu wa mawizara na taasisi mbalimbali na hata viongozi wateule, kwani kufanya hivyo kutapelekea mabadiliko makubwa katika taasisi za serikali na binafsi.

Mafunzo ya kujenga uwezo kwa watumishi wapya wa umma kwa kawaida hutolewa kila mwezi na Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), yakiwa na lengo la kujenga uweledi, uzalendo na maadili kwa watumishi wa Umma wa serikali na taasisi binafsi.