HAFSA GOLO NA MOHAMMED RASHID (DOMECO)

SERIKLAI ya Mapinduzi Zanzibar, imefafanua namna itakavyoimarisha uchumi wa nchi na watu wake kupitia dhana ya uchumi wa buluu iliyonadiwa na Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

Wakitoa ufafanuzi juu ya hoja za wajumbe wa baraza la wawakilishi walizozitoa wakati wakichangia bajeti kuu ya seriklai, baadhi ya mawaziri walisema mipango iliyoainishwa katika bajeti hiyo, imewekewa mikakati ya utekelezaji ili kuifanikisha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali, alisema ili kufanikisha mipango hiyo, serikali imejidhatiti katika ukusanyaji wa mapato lakini pia kuwa na nidhamu ya matumizi.

Aliongeza kuwa ili kupunguza ugumu wa maisha, serikali imeondoa na kusamehe baadhi ya kodi kwa wananchi wenye kipato cha chini ili waweze kumudu gharama za maisha.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha kauli ya ‘Yajayo ni neema tupu’ inatekelezwa na ndio maana imeamua kuondoa au kupunguza kodi katika baadhi ya maeneo ili kuwapa unafuu wa maisha wananchi wetu,” alieleza Jamal.

Aidha jamal alifafanua juu ya kodi ya majengo na kueleza kwa haitatozwa kwa kila nyumba bali zile zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50.

Aliongeza kuwa kifungu cha 28 cha sheria ya kumiliki mali namba 14/2008, kimeorodhesha aina ya majengo yaliyosamehewa kulipa kodi ya majengo hivyo wananchi wanapaswa kupuuza upotoshwaji unaofanywa.

“Kwa mujibu wa sheria, nyumba ambayo mmiliki wake anaishi ndani yake haitotozwa kodi hii kama ilivyo kwa majengo mengine ya umma, nyumba za ibada, kambi za jeshi na majengo ya taasisi za kimataifa,” aliongeza Jamal.

Akizungumzia marekebisho ya sheria ya kodi, Jamal alisema yanalenga kuimarisha biashara na kwamba viwango vya kodi ya ushuru wa forodha vitapunguzwa ili kuweka ustawi mzuri.

Awali Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Muhammed Mussa, alisema serikali itahakikisha hatua hiyo inatimia ipasavyo na kwa weledi kumalizia changamoto ya ukusanyaji mbaya wa mapato katika hoteli za kitalii.

alisema katika kuwadhibiti watendaji hao tayari serikali imeandaa mfumo wa kielektroniki ambao utakuwa na uwezo wa kudhibiti uvujaji wa mapato katika sekta ya Utalii.

Akizungumzia kuhusu miradi ya maendeleo katika sekta ya utalii alisema, serikali itaendelea kusimamia masuala ya ulinzi, ubadhirifu wa fedha huku ikihakikisha miradi yote inakua na ubora na kuleta maslahi maana kwa wananchi.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, alisema bajeti hiyo imeweka mikakati ya kuimarisha viwanda na biashara hivyo aliwaomba wadau wanaohusiana na eneo hilo kuunga mkono kwani imedhamiria kumalizia kilio cha muda mfrefu.

Alifahamisha kwamba hatua hiyo inakwenda sambamba na mipango ya kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika ambao utachochea masuala ya uwekezaji wa viwanda.

Nae Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum, alisema bajeti hiyo imeweka malengo mazuri ya uchumi na kufikia asilimia 5.2.Alisema ili kufikia hatua hiyo ni vyema kuwepo na usimamizi mzuri wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumzia kuhusu baadhi ya viwanda vinavyewekeza nchini alisema bado vimekuwa havizingatii suala la mazingira jambo ambalo linaleta changamoto katika mabadiliko ya uchumi.

Hivyo Waziri huyo alishauri watu wote wanaoekeza masuala ya viwanda katika maeneo ni vyema kufuata taratibu za kisheria.

Pamoja na hilo, alisikitishwa kuwepo kwa idadi kubwa ya vijana kutumia dawa za kulevya ambapo hadi sasa wamefikia 10,000.

Alisema hatua hiyo inachangia kupotea nguvu kazi ya taifa sambamba na kuhofia utekelezaji mzuri wa fursa za ajira laki 3 zinazotarajiwa kutolewa nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, alisema bajeti hiyo italeta matumaini mapya kwa wananchi na kuleta maendaeleo kwa zaidi ya asilimia 44.

Aidha alisema kuna mipango wa uimarishaji wa miundombinu ambapo bila ya shaka itaongeza hamasa katika uwekezaji.

Mjadala wa bajeti hiyo ulihitimishwa jana jioni na wajumbe walipitisha makadirio ya matumizi ya shilingi trilioni moja, bilioni mia nane na ishirini na tisa na milioni mia tisa (1,829.9 bilioni).

Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 947.1 ni kwa ajili ya kazi za kawaida na shilingi bilioni 882.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambapo pamoja na bajeti, baraza lilipitisha sheria ya kuidhinisha fedha ulipitishwa.