NA MWANAJUMA MMANGA

WAZAZI wa Wilaya ya Kusini Unguja, wametakiwa kushirikiana na walimu kufatilia maendeleo ya elimu kwa watoto wao, ili kuleta ufaulu mzuri katika mitihani ya ngazi mbali mbali ikiwemo ya taifa.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Rashid Makame Shamsi, aliyasema hayo wakati akizungumza na wazazi hao katika skuli ya Sekondari Makunduchi, ambapo alisema ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi ndio njia pekee itakayoleta matokeo  mazuri  na  kuondokana  na kuwa nyuma kielimu.

Shamsi alisema Wilaya hiyo imeandaa mikakati mbali mbali ya kuimarisha elimu kwa kuunda kamati zitakazoshirikiana na wadau wa elimu, ili kuhakikisha lengo la Wilaya hiyo linafanikiwa.

“Wazazi mnatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwashughulikia watoto wetu kujita katika suala zima la elimu kwa kuwa wao ni wapangaji wakubwa katika maendeleo.” alisema Mkuu huyo.

Nao wazazi hao walisema wako tayari kushirikiana na walimu na viongozi, ili kuona watoto wanafanya vizuri katika mitihani yao kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu Wilayani humo.

Walisema iwapo walimu na wazazi wakiwa kitu kimoja wataweza kunua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao sambamba na kuweka heshima skuli hiyo.