NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohamed, amewataka watendaji wa mabaraza ya Manispaa kukusanya kodi katika maeneo yote ya biashara yanayotambulika kisheria.

Waziri Masoud, alitoa tamko hilo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Madiwani wa Manispaa ya Magharibi ‘B’, ya kwamba kumekuwa na vikwazo kutoka taasisi za serikali vinavyowataka kutokusanya kodi katika baadhi ya maeneo ya biashara.

Alisema mamlaka ya kusimamia ukusanyaji wa mapato kwenye Manispaa na Halmashauri yapo katika Wizara inayosimamia Tawala za mikoa, hivyo ukusanyaji huo wa kodi huchangia katika mapato ya serikali.

Alisema kwa zile taasisi zinazokwepa kodi, serikali itahakikisha inazishughulikia, ili kwenda sambamba na dhamira ya serikali ya kulipa kodi kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Alisema serikali inapiga kelele juu ya rushwa, dhulma, urasimu, ubaguzi na mambo mengine yanayofanana na hayo kwani imetajwa kuwa ndio chanzo cha kuua uchumi nchini.

“Halafu hao hao ndio wanaosimama kifua mbele nakusema maendeleo hayaonekani kumbe ndio wakwepaji wakubwa wa kodi, hivyo vitendo kama hivi hatutoendelea kuvivumilia hata kidogo kila mtu ana haki ya kulipa na sio watu wachache”, alisema.

Aidha, Masoud aliwataka masheha na madiwani kushirikiana katika kuimarisha usafi katika maeneo yaliyowazunguka.

Alisema usafi ndio kila kitu katika maeneo yao kwani huweka haiba nzuri ya kuvutia sambamba na  kuondosha maradhi mbalimbali ikiwemo Kipindu pindu.

Wakizungumza katika kikao hicho baadhi ya Madiwani, wameomba kuwekwa mazingira mazuri yatakayowezesha watendaji wa Manispaa kufanyakazi zao kwa ufanisi.

Walisema bado wamekuwa na mazingira magumu ya kufanyia kazi na kushindwa kuwajibika vyema katika kazi zao za kila siku.