WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,  imekiri kuwepo malalamiko ya kutolipwa fedha za likizo kwa baadhi ya wafanyakazi wakiwemo waalimu.

Hayo yameelezwa katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar na Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Riziki Pemba Juma, kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, wakati akijibu suali la Mwakilishi wa jimbo la Uzini, Haji Shaaban Waziri, alietaka kujua kwanini waalimu hawapati fedha zao za likizo.

Waziri Pembe alisema kuwa hali hiyo imetokana na uhaba wa fedha za matumizi mengineyo, kwani hiyo ni haki ya kila mfanyakazi wa Serikali, ikiwa pamoja na waalimu.

Alisema Wizara imekuwa ikichukuwa hatua mbali mbali za kuhakikisha wafanyakazi wote wanalipwa posho lao kama sheria inavyoelekeza.

Hata hivyo, alisema Wizara imeandaa orodha ya watumishi wote wanaoidai maposho mbali mbali na itawalipa mara tu Wizara itakapopokea fedha kutoka mfuko mkuu wa Serikali kwani kwa mwaka 2020/2021 wapo  15 kwa Unguja na  920 kwa Pemba.

Aidha, alitaja sababu za Unguja kuwa na idadi ndogo ya wanaodai ni kwamba waalimu hao mwaka 2020, walilipwa posho la likizo, na kutokulipwa posho la usafiri, wakati Pemba walilipwa usafiri na hawakulipwa posho la likizo.