WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, itaendelea kufuatilia ajira za waalimu zitakazotolewa kwa lengo la kutatua changamoto la uhaba wa waalimu nchini.
Akijibu suali la mwakilishi wa jimbo la Mwambe, Mussa Foum Mussa, alietaka kujua serikali ina mpango gani kulichukulia hatua suala la uhaba wa waalimu, Waziri wa wizara hiyo Simai Mohammed Said, alisema uhaba wa waalimu ni suala ambalo linaendelea kuikabili skuli zao hasa za msingi ikiwemo ya Mwambe.
Alifahamisha Serikali inawaahidi wananchi wa jimbo hilo itendelea kutatua changamoto nyengine zinazoikabili skuli hiyo na skuli nyengine zote Unguja na Pemba.
“Kama ambavyo tulivyopunguza tatizo la uhaba wa nafasi skulini hapo kwa kujenga skuli moja mpya ya kisasa ya Sekondari na ndivyo tutakavyoendelea kutatua changamoto nyengine zinazoikabili skuli hiyo na nyengine zote za Zanzibar”, alisema.
Hata hivyo alisema skuli hiyo ya Mwambe ilikuwa chini ya mfumo wa ugatuzi, tayari imesharejea chini ya usimamizi wa wizara ya Elimu, hivyo aliahidi kufika skulini hapo kuangalia maendeleo na changamoto zinazoikabili skuli hiyo na kuzipatia ufumbuzi.