NA MWINYIMVUA NZUKWI

SERIKALI ya mapinduzi Zanzibar imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wamiliki wa hoteli za kitalii na wadau wengine ili kuimarisha utekelezaji wa dhana ya uchumi wa buluu.

Kauli hiyo imetolewa na rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na makamu wa pili wa rais, Hemed Suleiman Abdullah katika hafla ya uzinduzi wa jumuiya ya wenye hoteli Zanzibar (HAZ).

Dk. Mwinyi alieleza kwamba, kuna uwiano mkubwa kati ya sekta ya utalii na dhana hiyo hivyo mashirikianpo kati ya serikali na wadau wengine wakiwemo watoa hiuduma za fedha ni muhimu.

Alisema pamoja na kuwepo kwa maradhi ya corona, bado uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika kutokana na kuwepo kwa hoteli za kitalii zenye hadhi ya juu lakini pia huduma bora.

Alisema seriklai anayoiongoza itaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano kwa wadau wa sekta hiyo ili iendelee kuchangia uchumi wa Zanzibar na kuzalisha ajira kwa wananchi wake.

Aidha alipongeza dhamira ya jumuiya hiyo na kueleza kuwa itasaidia kutatua changamoto zinazowakabili na kuifanya iendelee kuwa imara.

Aidha alipongeza benki ya NMB kwa kutumia fursa ya uzinduzi wa jumuiya hiyo kurahisisha huduma zake zitakazochochea ongezeko la wageni na kutekeleza mikakati ya kufikia uchumi wa buluu.

Alisema, kitendo benki hiyo kuwa mdhamini mkuu wa hafla ya uzinduzi wa jumuiya hiyo, kinaonesha utayari wa benki hiyo kusaidia kukuza shuguli za utalii visiwani humo na kuiomba kufanya hivyo kwa wadau wengine wanaojihusisha na sekta hiyo.

“Uwekezaji wa hoteli unazidi kukua kwani dadi ya hoteli imeongezeka kwa kasi kutokan ambapo hoteli 509 mwaka 2018 hadi kufikia hoteli 620, sawa na ongezeka la hoteli kati 25 hadi 36 kwa mwaka,” alisema Abdallah.

Alibainisha kwamba ili serikali itimize malengo yake inategemea kwa kiasi kikubwa wawekezaji ambao nao hutegemea huduma bora zinazotolewa na wadau wanaochochea ukuaji wa sekta hiyo kukuza na kuanzisha biashara mpya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa HAZ, Paolo Rosso, alisema wana imani kubwa na kuishukuru serikali kwa kutoa msukumo maalum kwenye uwekezaji katika sekta ya utalii.

Alisema mazingira rafiki yaliyopo, yamechochea ongezeko la hoteli na watoa huduma wengine katika sekta hiyo jambo linalochangia ukuaji wa uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Aliongeza kuwa iumoja waliouanzisha utakuwa jukwaa litakalorahisisha majadilinano na kufungua njia ya kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta ya utalii.

Aidha Rosso aliishukuru benki ya NMB kwa kuwa karibu na wanachama wa jumuiya hiyo na kuiomba kuweka mifumo itakayosaidia kupata uwezeshaji lakini pia huduma bora kwa wageni wanaowahudumia.

“mashirikiano kati ya NMB, HAZ na seriklai yanatoa mwanzo mpya wa kuzikabili changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya hoteli hasa walkati huu wa covid 19,” alisema Mwenyekiti huyo.

Awali akitoa maelezo katika hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya serena Zanzibar, Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, alisema biashara ya hoteli inachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Zanzibar, hivyo anaamini taasisi yake ina fursa pana ya kibiasahara.

Alisema uwepo wa zaidi ya hoteli 500 zilizopo ikiwa ni sawa na zaidi ya vitanda 900, Zanzibar inaweza kupokea wageni wengi ikiwa kutakuwa na ubunifu wa kutosha.

“Kwa zaidi ya miaka 10, NMB imekuwa ikifanya vizuri katika biashara mfulululizo ni benki pekee inayotengeneza faida kubwa lakini pia imefika maeneo mengi Tanzania, hivyo tunaweza kutoa mkopo wa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mteja mmoja bila kutikisika,” alisema Mponzi.

Aliongeza kuwa, “Tumesikia pia kilio chenu wamiliki wa hoteli juu majanga ya moto na changamoto ya kutopata fidia kwa wakati, tunawahakikishia kuwa utaratibu wetu wa bima ni wa kipekee na una muhakikishia mteja kupata fidia yake yote kwa wakati”.

Alisema ili kuimarisha huduma, benki hiyo imefungua fursa pana kwa Zanzibar kwa kuweka mashine za kutolea fedha (ATM) 17 ambapo nyingine saba zitaongezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo inayotoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni itakayowekwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliomalizika kujengwa hivi karibuni.