NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, amesema wizara hiyo  itafanya mapitio ya sheria na kanuni  zenye mapungufu ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kutimiza azma ya serikali.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake Vuga kuhusiana na hatua zitakazochukuliwa katika utatuzi wa mgongano wa kisheria katika kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Alitaja baadhi ya sheria na kanuni zinazotarajiwa kufanyiwa marekebisho kuwa ni pamoja na sheria ya kuwaenzi viongozi wakuu wa serikali namba 1 ya mwaka 2015, sheria ya mfuko wa jimbo namba 4 ya mwaka 2012 na sheria ya kinga, uwezo na fursa ya Baraza la Wawakilishi namba 4 ya mwaka 2007.

“Tumedhamiria kuona sheria hizi zinakuwa na usimamizi bora na kuleta manufaa yaliyokusudiwa  na serikali kuliko ilivyo sasa,” alisema.

Kuhusu marekebisho ya kanuni, Waziri huyo alisema wamekusudia kufanya marekebisho ya kanuni ya sheria ya mfuko wa maafa, kanuni ya maafa na kanuni ya bendera ya Zanzibar ili kutoa muongozo katika utekelezaji wa sheria na kuleta ufanisi.

Alisema mtazamo na malengo  mengine  ni kuendana na mabadiliko ya ulimwengu wa sayansi na teknolojia na kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Aidha Waziri Khalid, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa watumishi wa umma na watendaji wa wizara hiyo, kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo yatakayorahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Sambamba na hilo, aliwataka wahakikishe wanasimamia majukumu ya kazi zao na kufanya kazi kwa uadilifu pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.