NA TATU MAKAME
WIZARA ya Habari,Vijana ,Utamaduni na Michezo imesema itahakikisha sekta ya michezo inaimarika na wizara kuisajili michezo yote nchini, ili kuweza kushiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje.
Kaimu Waziri wa Wizara hiyo Lela Mohamed Mussa alisema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, wakati akijibu suala la msingi lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni Shamata Shaame Khamis, aliyetaka kujua serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kuiinua michezo hiyo na kuipatia heshima kubwa nchini yao.
Alisema serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha mchezo wa riadha unarudi kama zamani, ambapo wanamichezo wengi walikuwa wanapata kushiriki na kushinda medali mbalimbali.
Alisema serikali imejenga viwanja vikubwa Unguja na Pemba vya Amaan na Gombani, kwa ajii ya kuinua michezo ikiwemo riadha kwa kukidhi viwango vya kimataifa.
Waziri Lela alisema katika kurejesha hali hiyo serikali kwa kushirikiana na chama cha riadha Zanzibar, kwa kurejesha utaratibu wa kuanzisha marathon kwa mwaka 2020-2021 ambayo ilikuwa ikifanyika kila ifikapo mwezi wa Novemba ya kila mwaka ,kwa kuimarisha na kuendeleza vipaji kwa vijana pamoja na kufufua vuguvugu la michezo.
Alisema kwa upande wa soka la ufukweni ZFF mwaka 2019 chini ya ibara ya 38 (13) ilianzisha kamati ya soka la ufukweni kwa kuinua mchezo huo,kamati hiyo pia ndiyo inajukumu la kusimamia mchezo huo kwa Unguja na Pemba na iliwahi kuwa bingwa wa mchezo wa soka la ufukweni na kupata kikombe na medali.
Alisema mpaka kufikia Machi 2021 baraza la michezo limesajili klabu za soka la ufukweni nane, tayari kwa sasa wapo baadhi ya wachezaji kutoka Zanzibar wameendelea na kambi ya timu ya taifa ya Tanzania itakayoshiriki mashindano ya Afcon 2021.
Waziri huyo alisema kwa upande wa mchezo wa Nage tayari baraza la taifa la michezo Zanzibar limechukua hatua ya kutambua na linaendelea na tataribu za usajili klabu za mchezo huo mpaka kufikia sasa jumla ya timu zipatazo 21 ambazo zinashiriki mchezo huo Unguja na Pemba.
Alisema taratibu za kufikisha usajili wa chama cha michezo wa Nage Zanzibar ili kuweza kusimamia mchezo huo unaendelea, na zinategemewa kukamilika hivi karibuni ili kuufanya mchezo huo kuwa na uongozi utakaoweza kuendeleza na kushajihisha jamii juu ya ushiriki wa ligi za mchezo wa nage hapa Zanzibar na kutambulika rasmin.
Hata hivyo alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha ya mwaka 2021-2022 ,Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kujenga viwanja vinne vya michezo hivyo sasa wanamichezo wataweza kunufaika kupitia viwanja hivyo na kuendeleza vipaji vyao.