NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan jana amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu ilisema Rais Xi Jinping amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua kijiti cha uongozi na kumpa pole kwa kuondokewa na Rais wa awamu ya tano hayati, Dk. John John Pombe Magufuli.

Taarifa hiyo ilisema katika mazungumzo hayo Tanzania na China zimekubaliana kukuza ushirikiano katika nyanja za uchumi, utamaduni na ushirikiano wa Kimataifa.

China imeahidi kufungua zaidi soko lake kwa bidhaa za Tanzania pamoja na kuongeza uwekezaji hususan katika sekta ya viwanda.

Aidha kupitia mazungumzo hayo China imeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Rais Samia Suluhu Hassan alitumia fursa ya mazungumzo hayo kutoa salamu za pongezi kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake na ameahidi kudumisha uhusiano wa kidugu na historia uliopo kati ya Chama hicho na Chama cha Mapinduzi (CCM).