NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

SIMBA na Yanga zimefanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano ya ligi kuu ya Vijana chini ya Umri wa miaka 20, inayoendelea kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Simba walifanikiwa kutinga nusu fainali kwa kuwachapa JKT Tanzania bao 1-0 huku Yanga wakitinga nafasi hiyo kwa kuwachapa Mwadui FC Mabao 3-0.

Kocha Mkuu wa kikosi cha Yanga U-20 Saidi Maulid, aliwapongeza wachezaji wake kwa hatua hiyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Alisema malengo yao nikutinga fainali na kubeba ubingwa wa bila kuangalia fainali watakutana na nani.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa hatua kubwa waliofikia, malengo yetu nikupata ubingwa wa ligi, bila kuangalia mpinzani wetu yupoje sisi tumejipanga na tunaweza kufanya hivyo,”alisema

Kwa upande wake kocha wa Simba U-20,Nickolaus baada ya kumalizika kwa mchezo wake alisema hakuna anaeweza kuwarudisha nyuma kwa hatua waliofikia.

“Nikweli tumepata ushindi mwembamba dhidi ya JKT Tanzania lakini hiyo haimaanishi tutashindwa kupata ubingwa,”alisema