ASYA HASSAN

WAKAAZI wa Shehia ya Unguja Ukuu Kaebona wameiomba Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kuweka watendaji wake katika maeneo ya kutolea huduma ili kudhibiti vitendo hivyo vya rushwa nchini.

Walieleza hayo katika mkutano wa kutoa elimu na kusikiliza kero za wananchi uliohusisha maofisa wa ZAECA na wakaazi wa kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Wananchi hao walisema ni vyema taasisi hiyo ikahakikisha katika maeneo muhimu ya kutolea huduma za jamii kama hospitali, mahakamani na sehemu nyengine kukawepo maofisa wa ZAECA, ili waweze kufuatilia utoaji na upatikanaji wa huduma hizo.

Mmoja ya wananchi hao Khalid Ali Sheha, alisema mara nyingi wananchi wakienda maeneo hayo hudhalilishwa kutokana na kutokuwa na uwezo na kusababisha kukosa huduma.

Hata hivyo, alifahamisha kwamba ni vyema serikali kupitia taasisi hiyo ikapanua wigo wa ufuatiliaji kwa kuweka maofisa wao katika taasisi hizo, ili kuwasaidia wananchi kupata huduma lakini pia kutoa taarifa zinazohusiana na watendaji wasio waaminifu.

Nae Ofisa Elimu kwa Umma kutoka katika taasisi hiyo, Saada Salum Issa, aliwataka wananchi wanapokwenda katika maeneo yoyote kutaka huduma kuhakikisha wanaipata bila ya usumbufu.

Alisema huduma zote zinatolewa kwa mujibu wa sheria na taratibu hivyo endapo wakibaini wanakosa huduma hizo hadi watoe fedha ni vyema wakaripoti sehemu husika ili wahusika wachukuliwa hatua stahiki.

Sambamba na hayo aliwataka wananchi kutoa mashirikiano kwa kuwaripoti wale wote wanaoonesha viashiria vyovyote vya kutaka rushwa katika utendaji wa kazi zao za kila siku za kuwatumikia wananchi.