NA ASIA MWALIM

CHAMA Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kimekusudia kuanzisha mfumo maalumu wa kuhifadhi taarifa za vitendo vya udhalilishaji ili kupata idadi sahihi za vitendo hivyo.

Mkurugenzi Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud, alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya utumiaji wa mfumo kwa waingizaji taarifa huko ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe Zanzibar.

Aidha Mkurugenzi huyo alisema uanzishwaji wa mfumo huo utaweza kuhifadhi taarifa halisi  za vitendo vya udhalilishaji na aina ya matukio yake kwa njia ya mtandao.

Alieleza kuwa kufanya hivyo ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, D.k Hussein Ali Mwinyi, katika kuhakikisha wanapunguza na hatimae kuondoa kabisa vitendo hiyo kwani matarajio yao ni kuhakikisha Mikoa yote inafaidika na kutumia mfumo huo wa mtandao.

Aidha alisisitiza wadau na wanachi mbalimbali kushirikiana na Chama hicho kwa lengo la kuisaidia jamii iweze kuondokana na kadhia hiyo, ambayo imeonekana ni kikwazo zaidi kwa wanawake na watoto.

Nae, Meneja wa Mradi huo, Salma Ali Bakari, alisema awali walikusanya maoni mbalimbali kutoka kwa taasisi binafsi na za kiserikali, hivyo kuona ipo haja ya kuharakishwa kuweka mfumo huo ikiwa ni hatua itayowaandolea usumbufu, pamoja na kupata takwimu sahihi kwa wanaharakati wakati wa kutoa taarifa hizo ambazo ni muhimu kuhifadhiwa.

Ramadhan Mohammed Ramadhan, alisema endapo watendaji wa vyombo vya sheria hawatatekeleza vyema wajibu wao ikiwemo kutoa ushahidi na hukumu zinazofaa, vitendo hivyo vitaendelea na kuengezeka siku hadi siku.

“Sisi tumeona ni jambo jema walilolianda ZAFELA, kikubwa mfumo ufanye kazi ili makosa yapungue” walisema.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalishirikisha wanaharakati mbalimbali wa vitendo vya udhalilishaji kutoka kisiwa cha Unguja na Pemba.