KAMPUNI ya ZAFICO inakusudia kujenga kiwanda cha kusarifu minofu ya samaki na vyumba vya baridi (An Intergrated Prosessing and Cold Storage Plant) katika eneo la Bandari ya Malindi.

Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Abdalla Hussein Kombo alisema hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani, wakati akijibu auala la msingi liloulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Mussa Foum Kombo alietaka kujua malengo ya kampuni hiyo.

Alisema pia ZAFICO inakusudia kujenga chelezo chake cha maegesho ya boti ZAKEV za uvuvi kando kando ya eneo hilo linalotarajiwa kujengwa kiwanda.

Aidha alisema hatua iliyofikiwa hadi sasa ni kukamilika kwa michoro ya mradi huo na kufanyika kwa zoezi la tahmini ya athari za kimazingira na kijamii (Environmental and Social Impact Assessment) na tayari nyaraka hizo zimeshawasilishwa kwa ZAFICO na Mshauri Elekezi.

Waziri huyo alisema kwa kuwa eneo hilo lipo katika eneo la hifadhi ya Mji Mkongwe, Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe waliishauri ZAFICO iwasilishe nyaraka na michoro ya mradi huo, ili kupelekwa UNESCO kwa kupatiwa (Approval).

Sambamba na hayo alibainisha kuwa mambo yote hayo yatategemea na matokeo ya upembuzi yakinifu yatakayoanisha uhalisia na gharama za ujenzi wa kiwanda pamoja na chelezo hicho.

Alisema jambo jengine pia ni mfumo wa mashirikiano baina ya serikali na wawekezaji kutoka sekta binafsi kupitia mpango unaopendekezwa na ‘Concessionary Agreement’.