NA JOSEPH NGILISHO ARUSHA

WAFANYAKAZI zaidi ya 125 wa hoteli maarufu ya kitalii ya Mount Meru jijini hapa wamelalamikia kuachishwa kazi kinyemela huku wakipunjwa madai yao ya Msingi, ikiwemo kiinua mgongo baada ya kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 na wamemwomba Rais Samia Suluhu kuingilia kati sakata hilo.

Wakiongea mapema leo baada ya kukabidhiwa barua za kufutwa kazi  wakiwa wamejikusanya nje ya lango kuu la kuingilia katika hotel hiyo, wamedai kwamba mwajiri wao amekiuka Sheria za kazi kwa kuamua kuwatimua kazi bila kuwapa notisi ya kuwajulisha nia yake mapema.

Yohane Malima ambaye alikuwa Meneja wa mikutano na matukio katika hotel hiyo, alisema kuwa mgogoro Kati ya wafanyakazi na mwajiri wao ulianza mapema mwaka Jana mwezi wa  tatu katika kipindi Cha mlipuko wa janga la Corona baada ya mwajiri kuamuru wafanyakazi kwenda likizo isiyo na malipo.

“Mwezi wa tano tuliamua kukutana wafanyakazi wote kutaka kujua hatima yetu lakini tulikubaliana kuendelea na likizo yetu isiyo na malipo baada ya kuona mwajiri hana ushirikiano na sisi”alisema.

Alisema ilipofika mwezi wa 11,mwaka jana waliamua kufungua shauri la madai tume ya Taifa ya usuluhishi na uamuzi(CMA)wakilalamikia mwajiri wao ,lakini wakati wanaendelea kusubiri hatima ya shauri hilo,wameshtushwa na hatua ya kupewa barua za kuachishwa kazi.

Kwa mujibu wa barua zilizoandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa hotel hiyo Andrew Strim,kwenda kwa wafanyakazi hao ,inaeleza kuwa sababu ya kuwapunguza kazi Ni kutokana na sababu za kiuchumi ikiwa Ni pamoja na mwenendo mbaya wa kibiashara .

Akiongea kwa njia ya simu Mmiliki na mkurugenzi wa hotel hiyo, Emanuel Wado(Sunda)alisema kuwa taratibu zote za kuwapunguza kazi wafanyakazi hao zimefuatwa, ila Kuna Kesi tatu wamefunguliwa mahakama zinaendelea”alisema Sunda kwa ufupi.

Mkurugenzi Andrew Strim, hakiweza kupatikana kuzungumzia madai hayo Hata alipopigiwa simu ya mikononi hakuonyesha ushirikiano baada ya kukata simu pindi mwandishi anapojitambilisha.