NA MADINA ISSA
KAIMU Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo, Lela Mohammed Mussa, amesema mpango wa kufufua mashindano ya mbio za Zanzibar International Marathon, unalenga kutangaza vivutio vilivyomo ili kuongeza idadi ya wageni nchini.
Akizindua mashindano ya kimataifa Zanzibar International Marathon huko Hoteli ya Park Hayat, alisema ili kuona dhana ya utalii kwa wote inafanikiwa ni vyema kubuni mambo yatakayoifanya Zanzibar kutajika zaidi duniani.
Alisema mashindano kama hayo yaliwahi kufanyika na Zanzibar kutambulika kimataifa,hivyo kuanzishwa tena kunahitaji mikakati imara ili kuwa endelevu.
Waziri Lela ambae pia ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, alisema serikali chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi ipo tayari kufanya kazi na sekta yeyote ikiwemo ya michezo, kwa nia ya kuinua uchumi wa nchi hasa ukizingatia kuwa lengo lake ni kupata medali 100 za dhahabu kupitia michezo mbali mbali.
Aidha alisema serikali inakusudia kuimarisha michezo mbalimbali ikiwemo Marathon na kuwapongeza waandaaji wa mashindano hayo, kwani wameonesha mwanzo mzuri wa kuona vipaji vinaonekana na vijana.
Sambamba na hayo, alisema kufanyika tamasha hilo kutapanua fursa ya kuutangaza utalii wa ndani kwa wazawa na nchi jirani kwani Zanzibar ni kisiwa cha utalii duniani.
Nae Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mashindano hayo, Hassan Suleiman Zanga, alisema mashindano hayo yana lenga kuunga mkono juhudi za serikali, katika kuitangaza Zanzibar ambapo amewahakikishia wageni kuwa Zanzibar itaendelea kuwa salama chini ya uongozi wake Dk. Hussein Ali Mwinyi katika fursa zinazotokana na uchumi wa buluu.
Aidha alisema kuna uhusiano mkubwa wa Marathon na utalii kwani michezo inawaleta watu pamoja, hivyo imani yao kuendeleza michezo mbalimbali,na aliiomba serikali kuendelea kuliunga mkono suala hilo ili kukuza michezo nchini.
Aidha alisema asilimia 20 ya fedha zitakazopatikana zitakwenda kwa wazee wa Zanzibar.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Fatma Hamad, alisema, kupitia wizara yao wataendelea kutoa mashirikiano ya hali ya juu ili kufanikisha mashindano hayo yanakwenda vizuri.
Pamoja na hayo, Katibu Fatma alifahamisha kupitia Marathon hiyo wataweza kuibua vipaji mbalimbali, pamoja na kujenga afya katika miili yetu.
Mashindano hayo ya kimataifa ya mbio Zanzibar yatahusisha mbio za kilomita 5, 10, na 21 ambapo wakimbiaji kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Zanzibar, Tanzania Bara, na nchi za nje zitakimbiwa kupitia maeneo mbali mbali ya mjini na kumalizia uwanja wa Amaan yanatarajiwa kufanyika Julai 18 mwaka huu.