NA AMEIR KHALID

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar inatarajia kupeleka wanamichezo kushiriki mashindano ya Umoja ya Michezo na Sanaa kwa skuli za Sekondari Tanzania (UMISSETA) mwezi huu.

Akizungumza na gazeti hili Mkuu wa Divisheni ya Idara ya Michezo na Utamaduni Wizara hiyo Dhihai Ali Dhihai, alisema watapeleka wanamichezo wanafunzi wa skuli za sekondari katika mashindano hayo.

Alisema mashindano hayo yatafanyika huko Mtwara kuanzia Juni 20 ambapo Zanzibar itawakilishwa na kanda ya Unguja na Pemba katika michezo mbali mbali.

Aliitaja michezo ambayo watashiriki wanamichezo hao ni mpira wa miguu, mpira wa mikono wanawake na wanaume, Riadha wanaume na wanawake, Wavu wanaume, Kikapu wanaume, Mpira wa Meza wanawake na wanaume, Sanaa.

Alisema jumla ya wanamichezo 1oo kutoka Unguja na Pemba 60 watashiriki.

Alisema tayari timu zote zimeanza mazoezi pamoja na kucheza michezo mbali mbali ya kirafiki, lengo kufanya vyema na kurudi na vikombe katika mashindano hayo.

Aliongeza kuwa mashindano hayo yataanza Juni 20 na wanamichezo wa Zanzibar wanatarajia kuondoka Juni 18 kuelekea Mtwara kwenye ngarambe hizo.

Kuelekea mashindano hayo Dhihai aliongeza kuwa wanatarajia kufanya vyema na kurudi na vikombe na medali kama yanavyofanya miaka yote, kutokana na maandalizi ya muda mrefu waliofanya.