NA MADINA ISSA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya nchini.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Migombani, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa dawa ya Kulevya, Luteni Kanali Burhani Zubeir Nassoro, alisema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Juni 26 katika ukumbi wa Sheikh Irisa Abdulwakil, Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema dawa za kulevya ni tishio kubwa ambalo linaloendelea kuleta madhara duniani ambapo Zanzibar imekuwa ni waathirika kwa kiwango kikubwa.

Alisema nchi za Afrika Mashariki na Kusini imebainika kuwa ni njia kuu zinazopitisha dawa za kulevya ambapo kwa Zanzibar kila eneo ni mlango wa kuingia Zanzibar ambapo hakuna mlango maalum unaosababisha vijana wengi kuathirika na madawa hayo.

Alisema ni vyema jamii kuchukua hatua madhubuti ya kuhakikisha kwamba jamii inadhibiti madawa ya kulevya ambapo Zanzibar bila ya madawa ya kulevya inawezekana ambapo jamii ikishirikiana na kushajihishana pamoja na kubadilisha mifumo ambayo waliyokuwa wakiishi.

Aidha alisema, tume hiyo imejipanga kushirikiana na wadau wa sekta mbali mbali kuhakikisha wanafikia lengo la serikali juu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.

Alisema dawa za kulevya ni miongoni mwa mambo yanayoathiri kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya taifa na kuzorotesha maendeleo kutokana na kuathirika kwa wingi vijana na watu wazima wenye uwezo wa kufanya kazi.

Luteni Kanali Nassoro aliongeza kuwa takwimu kutoka kitengo cha kupambana na dawa za kulevya cha polisi zinaonesha kuwa kipindi cha miaka 9 (2012 – 2020) watuhumiwa wanawake na wanaume 3,810 walikamatwa kwa kujihusisha na uhalifu wa dawa za kulevya hali inayoonesha sio nzuri kwa sasa.

“Athari za dawa hizi ni kubwa sana hasa kwa vijana hivyo ni vyema jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa tume hii ili kuona wote watakaohusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki,” alisema.

Sambamba na hayo, alisema kuwa tume hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa dawa za kulevya kwa Zanzibar inakuwa historia na kuwataka wadau wa mapambano hayo, kuhakikisha watuhumiwa wanaokamatwa hawapewi dhamana.

“Tume imejipanga kuthibiti dawa hizo kuingia nchini kwani athari ya dawa hizo ni kubwa zaidi kwa vijana hivyo tunaishauri jamii kutoa ushirikiano kwa taasisi zinazohusika na vita hii,” alieleza Nassor.

Aliongeza kuwa ingawa maumbile ya visiwa vya Zanzibar kijiografia bado yanaleta ugumu katika kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya   hasa katika maeneo ya mipakani na bandari zisizo rasmi.

Aidha Luteni Kanali Nassoro, aliwataka wadau wakiwemo viongozi wa wilaya, mikoa na serikali kuu kutolifumbia macho suala la dawa za kulevya kwa kuwa wawazi ili kuendana na kaulimbiu ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya inayosema; ‘Sema ukweli juu ya athari za dawa za kulevya okoa maisha’.