NA RUKKAIYA MAHMOUD, ZHC

SHIRIKA la Nyumba Zanzibar, (ZHC) limesaini mikataba ya ukodishwaji wa Nyumba za Makaazi baina yake na Kampuni ya Mardev Limited ya Morocco.

Mikataba hiyo ilisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mwanaisha Alli na Shahidi wake Ofisa Sheria, Taufik Bushir na upande wa kampuni ya Mardev Limited, ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Omar Mouline na Shahidi wake Mwanasheria Ibrahim Jaffar.

Taarifa kutoka katika Shirika hilo zilizotolewa na Ofisa Uhusiano, Rukkaiya Mahmoud, alisema Mkataba huo umetiwa saini katika ofisi zao Vuga Mjini Zanzibar, ambapo nyumba hizo zitaikodisha kampuni ya Mardev Limited yenye makaazi yake Morocco Nyumba zake nne.

Alisema nyumba hizo zenye namba 288-289 ziliyopo Hurumzi, ambapo nyengine ni namba 291 ya Forodhani, 291B ya Forodhani pamoja na 292B ya Kiponda.

Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar, Mwanaisha Alli Said, alisema Nyumba hizo zimekodishwa kwa kampuni hiyo kwa ajili ya maakazi na wamepatiwa mkataba huo baada ya kufikia makubaliano yote pamoja na kuwalipa waliokuwa wapangaji wa nyumba hizo awali.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo, alisema mara tu baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo mpangaji huyo ataruhusika kutumia nyumba hizo. Pia aliwasisitiza Mardev Limited kuzitunza pamoja na kufuata na kutii masharti ya mikataba hiyo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mardev Limited, Omar Mouline amelishukuru Shirika kwa ushirikiano wote uliofanikisha kuwepo kwa mkataba huo.