NA HABIBA ZARALI
JUMUIYA inayosaidia watu wa makundi maalum, Zanzibar International Development Organization (ZIDO) imetoa msaada wa chakula, vifaa vya kujisitiri ikiwemo kofia na miwani kwa watu wenye ualbino kisiwani hapa, ili kusitiri ngozi zao zisiathiriwe na na jua.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo katika skuli ya sekondari Madungu, Chake Chake, Maimuna Omar Said, alisema kofia na miwani
itawanusuru wasiathiriwe na jua kwani wameshindwa kupata vifaa hivyo kwa muda mrefu.
Alifahamisha kuwa mionzi ya jua kwa watu wenye ualbino inawaathiri na mara nyingi hupata matatizo ya macho na ngozi jambo ambalo huwaweka katika hali mbaya kiafya.
“Watu wenye ualbino tunaumia sana tunapokosa kofia, miwani pamoja na losheni na hutufanya tukae ndani ili jua lisituumize na hii inakuwa ni shida kwetu lakini huwa hatuna la kufanya,”alisema Maimuna.
Rabia Ali Salim wa Chake Chake, alisema watu wenye ualbino kisiwani hapa wameathirika ngozi na wengine wamefanya vidonda jambo ambalo kwa sasa litapungua baada ya kupata vifaa hivyo.
Alieleza walioathirika wengi wao ni watoto, kwani huwa hawajui kujilinda na kuwataka wazazi wa watoto hao kujitahidi kuwatunza, ili waishi kwa usalama.
Ofisa afya wilaya ya Wete, Mwarabu Nuhu Mwarabu alifahamisha kuwa kofia, miwani na losheni maalum ya kuzuia jua kwa wenye ualbino inasaidia mionzi ya jua isipenye kwenye ngozi zao.
Alifahamisha kuwa mtu mwenye ualbino anapopigwa na jua ngozi yake huharibika kwa kufanya vidonda vyenye maumivu na baadae husababisha saratani ya ngozi jambo linalowafanya wateseke na baadhi yao kufupisha maisha.
“Watu hawa wanahitaji uangalizi mzuri hasa wanapokuwa wadogo na wanashauriwa kuvaa nguo nyeupe, ili waweze kutimiza yale masharti yanayowafanya wajikinge na jua na kubaki salama,”alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya watu wenye ualbino Pemba, Mudathir Sharif Khamis, alisema, fursa waliyoipata kutoka jumuiya ya ZIDO ni adhimu kwao kwani imeonesha kuguswa na kuwajali kwa kuwapa mahitaji kama wanavyowapa wengine.
Rais wa jumuiya hiyo, Rehana Merali kutoka nchini Canada, alisema, jumuiya hiyo imejikita zaidi katika kusaidia watu wa makundi maalum wakiwemo yatima, wenye ulemavu, wazee na wajane ambao mara nyingi wanakuwa na hali ngumu za maisha.
Alifahamisha kuwa wananchi wenye mazingira magumu wanahitaji kusaidiwa katika hali tofauti, hivyo ni jambo la busara kila mwenye uwezo akasaidia ili watu wote wakawa katika hali moja na njema.
Mkuu wa jumuia hiyo kwa upande wa Zanzibar, Makame Ramadhan, alisema, wamegundua kuwa wapo wazazi wanawafungia ndani watoto wenye ualbino na kuwakosesha riziki zao, hivyo ni vyema kuacha tabia hiyo kwani nao ni watu kama walivyo wengine.