Na Ali Shaaban Juma

Usafiri  wa  majini ulianza karne nyingi zilizopita ambapo watu katika sehemu mbalimbali ulimwenguni walisafiri kutoka eneo moja hadi jengine kwa sababu mbalimbali. Tunapozungumzia usafiri wa majini tunakusudia usafiri wa vyombo vinavyoelea na kusafirisha abiria na mizigo katika maziwa, mito na bahari.

Kumbukumbu  za historia zinaonesha kuwa usafiri wa baharini ulianza karne nyingi, lakini usafiri wa meli kubwa za abiria zilizovuka bahari kuu na kusafirisha abiria wengi ulianza  hapo mwaka 1831.

Baada ya kuvumbuliwa bara la Amerika na Marekani kuanza kupata nguvu za kiuchumi mwishoni mwa miaka ya 1800, watu wengi walihama barani ulaya na kwenda Marekani kutafuta maisha mapya.

Kutokana na msukumo huo, makampuni ya usafirishaji abiria baharini yalitengeneza meli kubwa kwa ajili ya kuvusha abiria kutoka barani Ulaya kwenda Marekani na Canada.

Meli kubwa ya kwanza ya abiria iliyosafirisha abiria kati ya bara la Ulaya na Bara Amerika kwa kuvuka bahari kuu ya Atlantiki ilikuwa ni  S.S Royal  William iliyotengenezwa nchini Uingereza.

Meli hiyo iliyotumia makaa ya mawe ilikuwa na urefu wa mita 49, uzito wa tani  1,370 na uwezo wa kuchukua abiria 155. Meli hiyo iliyofanya kazi ya kuvusha abiria na mizigo kati ya Ulaya na Bara Amerika kwa miaka sita kati ya mwaka 1831-1836. Meli hiyo ya kampuni binafsi iliyosajiliwa nchini Canada ilizama mwaka 1860.

Meli ya pili ya abiria kubwa duniani ni ile iitwayo S.S. Great Western iliyotengenzwa makusudi kwa ajili ya kusafirisha abiria kutoka barani Ulaya kwenda Marekani kwa kuvuka bahari kuu ya Atlantiki.

Meli hiyo iliyomilikiwa na kampuni ya “Great Western Steamship Company”  ilikuwa na urefu wa mita 77, uzito wa tani 1,340 na uwezo wa kuchukua abiria 128. Ilikuwa na wafanyakazi wa kawaida 20 na mabaharia 60. Meli hiyo iliyosajiliwa nchini Uingereza ilifanya kazi kwa miaka miwili tu kati ya mwaka 1837-1839 na ilikatwa vipande vya chuma chakavu hapo mwaka 1855.