CAIRO, Misri
MIAMBA ya Zamalek imetangaza rasmi kuwa mchezaji wa kimataifa wa Misri, Ahmed Sayed Zizo, amesaini kandarasi mpya na klabu hiyo hadi 2025, akiwa mchezaji wa pili kukubali mkataba mpya baada ya Mahmoud Hamdy El-Wensh.
Licha ya kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Zamalek tangu asaini kwao mwaka 2019, Zizo amekuwa akitajwa kuondoka huku akizivutia klabu kadhaa za Ghuba na miamba ya Cairo, Al Ahly.
Zizo amekamilisha mechi 100 akiwa Zamalek wiki iliyopita dhidi ya Aswan. Katika kipindi chake chote ametoa michango 30 ya magoli [mago 15 na usaidizi 15] na kuwaongoza miamba hiyo kutwaa mataji manne, Kombe la Shirikisho la CAF, Kombe la CAF Super Cup, Kombe la Misri na Kombe la SuperCup la Misri.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliahidi utii wake kwa Zamalek na akaelezea azma yake ya kubakia klabuni hadi atakapostaafu.
Weupe hao walichukua hatua hiyo na kufanikiwa kupata makubaliano ya kuongeza kandarasi ya Zizo hadi Juni 2025, baada ya mkataba wake wa sasa kukamilika majira ya joto ijayo.
“Ilikuwa muhimu kuendelea na utumishi wangu na Zamalek, kila mtu anajua kiwango cha shinikizo nililokuwa nikipata hivi karibuni”, Zizo aliiambia televisheni ya Zamalek.
Zizo pia amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha timu ya taifa ya Misri cha Hossam El-Badry, kwani ameitwa kwa kila kambi tangu Novemba 2019. Lakini, bado hajafunga bao lake la kwanza la kimataifa.(Goal).