kufungua vituo ulipaji kodi hadi vijijini
NA KHAMISUU ABDALLAH
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema dhamira yake ni kufungua vituo vyake vya ulipaji kodi katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini, ili kuimarisha huduma za ukusanyaji wa mapato.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa Uhusiano Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Makame Khamis Mohammed, wakati akizungumza katika mkutano uliowashirikisha madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kati huko Dunga.
Alisema kuanzishwa kwa kituo cha ulipaji kodi katika kijiji cha Paje, na maeneo mengine kutarahisha ulipaji kodi wa hiari na kuongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato ya serikali nchini.
Aidha alisema hatua hiyo pia itasaidia wananchi wa maeneo ya vijijini kuepuka usumbufu wa kufuata huduma hiyo mjini.
Hata hivyo, alisema azma serikali ni kuhakikisha inawajengea mazingira mazuri wafanyabiashara mbalimbali ili kuona wanalipa kodi kwa wakati na serikali kupanga mikakati yake ya maendeleo nchini.
Hivyo, aliwataka madimani hao kushirikiana na bodi hiyo katika kuhamasisha wananchi juu ya suala la kudai risiti pale wanapofanya mauzo ili kuepusha miaya ya upotevu wa mapato ya serikali.
‘Sisi ZRB tunajitahidi kutoa elimu katika suala hili na tunaendelea kutoa elimu hivyo nanyi mtuunge mkono kwani bado wananchi hawajahamasika katika suala la kudai risiti pale wanapofanya manunuzi hali ambayo inasababisha mapato mengi ya serikali kupotea kiholela,” alisisitiza.
Nae Badria Attai Masoud kutoka bodi hiyo aliwaomba madiwani hao kuisadia ZRB kufichua matatizo mbalimbali ndani ya wadi zao ikiwemo, wafanyabiashara ambao wanafanya biashara zao kinyume na sheria na utaratibu unaotakiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza Mji Kati Said Shabaan Hassan, aliipongeza bodi hiyo hiyo kuanzisha kituo hicho kwani kufanya hivyo kumewapuzingia gharama wananchi kuzifuata huduma hizo mjini.
Alisema ni vyema bodi kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananch juu ya umuhimu wa kujisajili wakati wa kuanzisha biashara zao ili waweze kulipa kodi ya serikali.
Nao madiwani hao waliiomba ZRB kuandaa mpango maalumu wa kuwatoza kodi wafanyabiashara wa gari ili na wao kutoa kodi kama wafanyabiashara wengine nchini.
Diwani wa Viti Maalum Tendani Mkanga Miraji alisema hivi sasa watu wengi wamekuwa wakitumia gari aina ya keri kufanya biashara zao na wanapata fedha nyingi hivyo ni vyema kuliangalia jambo hilo.
“Ni kweli wafanyabiashara wa magari haya na mengine kuna kodi kubwa ambayo inakosekana pale kwani wanapata fedha hivyo hawashindwi kulipa kodi ambayo ni muhimu kwa maendeleo kwa jamii,” alisisitiza.