KAMPALA, UGANDA
TAARIFA kutoka nchini Uganda zinaeleza kuwa zaidi ya watu 800 na idadi kadhaa ya wateja kampuni mbalimbali katika jiji la Kampala wamedungwa sindano za chanjo bandia ya ugonjwa wa corona.
Hayo yamebainika kufuatia mamlaka za serikali nchini humo kufanya vipimo vya uchunguzi kwa kuchukuliwa sampuli za chanjo waliopatiwa watu hao.
Mkurugenzi wa kitengo cha uangalizi wa afya katika ikulu ya nchi hiyo, Dk. Warren Naamara, alivieleza vyombo vya habari kuwa, watuhumiwa waliofanya utapeli huo wanatafutwa ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Dk. Naamara alisema daktari aliyehusika kwa utapeli huyo bado hajafamika ambapo uchunguzi rasmi umeanza dhidi ya tukio hilo.
Alisema katika tukio hilo wananchi waliokuwa wakihitaji kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa corona walidungwa sindano zenye dawa bandia tukio ambalo lilitokea kati ya Mei 15 hadi Juni 17 mwaka huu.
Alisema chanjo walizopewa watu hao zilichanganywa na nyengine halisi zilitumwa maabara ya uhakiki ya Kurugenzi ya Serikali iliyoko Wandegeya na kwa Mamlaka ya Taifa ya Dawa ya nchi hiyo (NDA), kwa ajili ya uhakiki kabla ya kusafirishwa na kupelekwa India ili kufanyiwa ulinganishaji na chanjo halisi za Covid-19.
Taasisi ya Serum ya India iliyotengeneza chanjo za corona zilizotumwa nchini Uganda ilithibitisha kuwa chanjo hizo zilizotiliwa shaka hazikusafirishwa na taasisi hiyo kutumwa nchini humo.
Dk. Naamara alibainisha kuwa, kutokana na uhakiki wa mada zilizomo ndani yake, chanjo hizo bandia zilikuwa zimejazwa maji zaidi ya kitu kingine chochote kile.
Hata hivyo alisema, watu waliopigwa chanjo hizo bandia hawajatiwa miilini mwao kitu chochote chenye sumu au kuhatarishwa maisha yao.
Hadi sasa makachero wa ikulu ya rais wa Uganda wameshawatia mbaroni wauguzi wawili kutoka Nakawa, Kampala wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.