NA ASYA HASSAN

WATU watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokea ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja, ndani ya kipindi cha wiki moja.

Akizungumza na Zanzibarleo Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Suleiman Hassan Suleiman, alisema marehemu hao kuwa ni Haji Maulid Vuaa (50) mkaazi wa Dunga Kiembeni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo marehemu huyo alifariki dunia baada ya kuanguka na mnazi.

Alifahamisha kuwa tukio hilo limetokea Julai 25 ya mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi huko Dunga Kiembeni ambapo marehemu huyo alipanda mnazi kwa ajili ya kuangua nazi na baada ya kufika masafa uling’oka na kuanguka.

Alisema kitendo hicho kilisababisha marehemu huyo kupata majeraha mbalimbali ndani ya mwili wake na kukimbizwa hospitali kuu ya Mnazimmoja na kufariki dunia akiwa anapatiwa matibabu.

Kamanda Suleiman, aliwataja marehemu wengine kuwa ni Mabruk Said Omar (23) mkaazi wa Misufini wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, na mwanaume ambae hakufahamika jina lake anaekisiwa kuwa na umri kati ya miaka (25).

“Watu hawa walifariki dunia wakiwa hospitali kuu ya Mnazi mmoja wakipatiwa matibabu baada ya gari waliyokuwa wakisafiria aina ya Noha yenye namba za usajili Z. 597 FM kupinduka huko maeneo ya Dunga Jeshini,”alisema.

Aidha alifahamisha kwamba tukio hilo limetokea Julai 23 mwaka huu majira ya saa 7:30 usiku, ambapo alimtaja dereva wa gari hiyo kuwa ni Mabruk baada ya kufika eneo hilo gari hiyo ilimshinda na kupinduka na kusababisha vifo vyao yeye na mwenzake waliokuwa wamekaa mbele.

Aliwataja watu wengine waliyopakiwa katika gari hiyo kuwa ni Anjeli Logan (28) mkaazi wa Kwamchina Mwanzo Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, Salma Hamad Yusuf (29) mkaazi wa Darajabovu wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, ambao majeruhi hao wapo hospitali ya Mnazimmoja wanaendelea na matibabu.