CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI
SERIKALI ya Afrika Kusini imepanga kuwapeleka wanajeshi 25,000 kudhibiti ghasia zilizodumu kwa muda wa siku sita mfululizo.
Inaelezwa kuwa watu 72 wamekufa na wengine zaidi ya 1,200 wamekamatwa katika maandamano ya kupinga hatua ya rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma kufungwa miezi 15 jela.
Aidha serikali ya nchi hiyo imesema matukio 208 ya uporaji na uharibifu yamerikodiwa, huku idadi ya wanajeshi waliosambazwa ikiongezeka mara mbili hadi kufikia 5,000.
Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Novisiwe Mapisa-Nqakula ameliambia bunge kwamba amewasilisha ombi la kupelekwa wanajeshi 2,500 wa ziada.
Rais Cyril Ramaphosa ameidhinisha kusambazwa wanajeshi ili kuwasaidia polisi.
Aidha hadi sasa Novisiwe hajasema ni lini wanajeshi hao watapelekwa mitaani.
Hata hivyo Rais Ramaphosa amekutana na viongozi wa kisiasa na kuwaonya kwamba baadhi ya maeneo ya nchi huenda yakakosa huduma muhimu kutokana na kuharibiwa kwa mfumo wa kusambaza chakula, mafuta na dawa.