NA MARYAM HASSAN

LICHA ya kuwasilisha mashahidi watatu wa kumtetea katika mashitaka aliyoshitakiwa nayo ikiwemo kubaka, kutorosha na kuingilia kinyume na maumbile amehukumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka 30.

Mashahidi hao waliwasilishwa na mshitakiwa Shaibu  Ame Omar (34) mkaazi wa Koani ambao walionekana kuwa pamoja na mshitakiwa huyo lakini ushahidi wao haukuweza kuupingana na maelezo yaliyotolewa na shahidi wa upande wa mashitaka.

Katika kutafuta haki wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Shumbana Mbwana aliwasilisha mashahidi sita ambao walithibitisha kosa la mshitakiwa huyo.

Kabla ya kupewa adhabu hiyo mshitakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa tayari ameshakaa sana gerezani.

Mshitakiwa lishitakiwa kwa kosa kumtorosha msichana aliyechini ya uangalizi wa wazazi wake, ametenda kosa hilo mnamo mwezi wa tisa mwaka 2019 majira ya saa 7:00 za mchana huko Koani wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa bila ya halali alimtorosha mtoto wa kike mwenye umri wa miaka (10) ambae bado yupo chini ya uangalizi wa wazazi wake kutoka nyumbani kwao Koani na kumpeleka nyumani kwake huko huko Koani kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Aidha mshitakiwa alishitakiwa kwa kosa la kumuingilia mtoto huyo katika sehemu zake za siri za mbele kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo pia anadaiwa kumuingilia mtoto huyo kinyume na maumbile kosa hilo pia anadaiwa kuteda siku hiyo hiyo kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Adhabu kwa mshitakiwa huyo imetolewa na Hakimu Saidi Hemed Khalfan , baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa

Hakimu Said alisema mshitakiwa kwa kila kosa alitakiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka 10 huku adhabu kwa mshitakiwa ziende sambamba.

Hivyo mshitakiwa kwa makosa yote aliyoshitakiwa nayo atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka 10.Pia mshitakiwa ametakiwa kulipa fidia ya shilingi 3,000,000 kwa mhanga wa tukio hilo