NA SABRA MAKAME, (SCCM)

WATU 23 wamashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi kwa tuhuma mbali mbali ikiwemo mmoja kukutwa na lita 220 za mafuta ya Diseli.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP, Awadh Juma Haji, aliyasema hayo ofisini kwake Mwembemadema wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya matukio yaliotokea Mkoa wake kwa kipindi cha wiki moja iliyopita.

Alisema katika operesheni iliyofanywa na jeshi hilo kuanzia Julai 7 hadi 13, mwaka huu, lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 12 wakiwa na mafurushi 28 na nyongo 360.

Aidha, alisema katika operesheni hiyo pia walifanikiwa kukamata watu tisa pamoja na lita 46 za pombe ya kienyeji na mtambo mmoja wa kufanyia pombe hiyo.

Kamanda Awadh, alibainisha kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo mbali mbali ndani ya mkoa huo kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo uuzaji wa dawa za kulevya, utumiaji na usambazaji wa dawa za kulevya.

Akiwataja baadhi ya wathumiwa hao alisema ni pamoja na Farid Nasri Said (24) mkaazi wa Mpendae, ambae alikamatwa Julai 7 mwaka huu, majira ya sa 2:00 usiku, huko maeneo ya Masingini akiwa na kete 180 za dawa ya kulevya aina ya heroine.

Mtuhumiwa mwengine alisema ni Amini Hamad Mzee (54) mkaazi wa Mwanyanya akiwa na mafuta ya Disel lita 220 zikiwa ndani ya madumu 11 yenye ujazo wa lita 20 kila moja ambayo inadhaniwa kuwa ni mali ya wizi.