MOGADISHU, SOMALIA

MWANAUME mmoja nchini Somalia ameuawa kwa kupigwa risasi, huko kusini mwa nchi hiyo na serikali ya Jimbo la Jubaland baada ya kumbaka binti yake wa kambo mwenye umri wa miaka mitatu ambaye alifariki kutokana na majeraha ya kubakwa.

Mahakama katika mji wa Dhobley imemkuta Hussein Adan Ali mwenye umri wa miaka 28 na hatia hiyo siku ya Jumatano, kama ilivyotangazwa katika kituo cha televisheni cha eneo hilo.

Inaelezwa kuwa viongozi wa jadi na maofisa wa mahakama walipitia ushahidi kabla ya kutekeleza hukumu hiyo, huku ikielezwa kuwa Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa, Ali alikuwa amekula mirungi wakati alipomfanyia unyanyasaji huo mtoto wake.

Licha ya kutowekwa wazi tukio hilo lilipotokea, lakini mahakimu wamesema mtoto amefariki Jumatano.

Aidha matangazo ya Televisheni hayakuonesha kama mawakili walihudhuria mahakamani au mshutumiwa kama alipata fursa ya kukata rufaa, ila mahakama ilisema kuwa hukumu hiyo ya kifo ilitolewa chini ya sheria za kiislamu.

Pia televisheni ya taifa ya Somalia iliweka picha ya Ali katika kurasa wake wa twitter.