ZASPOTI
TIMU ya taifa ya Argentina imetwaa taji la michuano ya Copa America baada ya ushindi wa goli 1-0 mbele ya Brazil katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro.

Ubingwa huo ulihitimisha kusubiri kwa Lionel Messi kwenye kutwaa taji lake la kwanza la kimataifa akiwa na Argentina katika kipindi cha miaka 10.
Kiungo, Angel Di Maria alipachika goli hilo la ushindi kwenye dakika ya 22 ambalo lilidumu mpaka dakika ya 90 ya mchezo huo uliokuwa mkali na wenye ushindani.

Mchezo huo ulitazamwa na umati mdogo wa wageni waalikwa 7,000, kwa sababu ya vizuizi vya maambukizi ya ‘corona’, lakini, ulikuwa wa kwanza wa mashindano kuwa na watazamaji.

Imekuwa miaka 15 tangu Messi awakilishe Argentina kwa mara ya kwanza kwenye mashindano makubwa na baada ya Kombe la Dunia mara nne na mara sita za Copa America, akichukua mechi 53, mwishowe ana taji kuu la kimataifa yeye na nchi yake.

Licha ya kuwa mmoja wa wachezaji waliopambwa na mahiri wa enzi ya kisasa na wakati wote na mataji 10 ya ‘La Liga’, manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na tuzo sita za Ballons d’Or, maswali juu ya ukosefu wake mafanikio kwenye hatua ya kimataifa yametanda juu ya urithi wake.

Wenyeji Brazil ndiyo walionekana kumiliki mchezo ambapo walipiga mashuti 13 huku mawili yakilenga lango wakati Argentina ilipiga mashuti sita.
Ikiongozwa na nyota wao, Neymar Jr., Brazil ilijitahidi kupambana na Argentina ilioyoongozwa na Messi.

Ilikuwa ni fainali ya kibabe ambayo ilishuhudia kadi tisa za njano zikitolewa ambapo Argentina walionyeshwa tano na Brazil nne.
Kabla ya fainali hiyo, miamba hiyo ilishakutana mara 33, Argentina ikishinda mechi 13, Brazil mechi 10 wamekwenda sare mara mane.

Bado kuna matarajio ya Messi kwenda kutumia fursa yake labda ya mwisho kushinda Kombe la Dunia – jambo ambalo Argentina hawajafanya tangu 1986 – ikiwa ataiongoza nchi yake kwenda Qatar akiwa na umri wa miaka 35 mnamo Disemba 2022.(AFP).