SMZ yawatoa hofu wananchi

NA MWANAHAWA HARUNA

ZOEZI la utoaji wa chanjo ya Kipindupindu lilioanza Julai 3, 2021 limeonyesha kufanikiwa kwa asilimia 60 kupata tiba hiyo, baada ya wananchi kujitokeza katika vituo, katika vituo mbali mbali vilivyowekwa kwa Unguja na Pemba.

Mkurugenzi Kinga Wizara ya Afya, Fadhili Mohammed Abdallah, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo, juu ya zoezi hilo huko Ofisini kwake  Hospitali ya Mnazimmoja Mjini Unguja.

Mkurugenzi huyo alisema amewatowa ghofu wananchi juu ya chanjo ya Kipindupindu inayoendelea kutolewa katika baadhi ya shehiya hapa Zanzibar kwani zoezi hilo linaenda vizuri na tayari limefikia asilimia (60) ya zoezi hilo ambalo wanatarajia kuzidi kwa kiwango hicho baada ya kumalizika kwake.

Alisema kumekuwa na uvumi unaondelea juu ya chanjo ya Kipindupindu iliyoanza kutolewa hivi karibuni katika visiwa vya Unguja na Pemba ina madhara kwa uzazi huku wengine wakidai ni ya korona .

Amesema chanjo hiyo imefanyiwa utafiti mbali mbali na kuonesha kuwa haina madhara yeyote kwa Watumiaji , na kuwaomba wananchi wasiwe na wasi wasi na chanjo hiyo.

Alieleza kuwa kabla ya chanjo hizo kutumika hapa nchini lazima ziwe zimekaguliwa na tasisi mbalimbali za kiserekali ikiwemo Taasisi ya Viwango Zanzibar,  (ZBS) ambazo zitazothibitishwa kuwa hazina madhara.

“Chanjo ya Kipindupindu sio mara ya kwanza kutolewa duniani na si mara ya kwanza kutolewa Zanzibar, iliwahi kutolewa mwaka 2009, katika baadhi ya shehiya sita wakati huwo na kutoripotiwa kesi ya Kipindupindu kwa muda wa miaka mitano katika shehiya hizo” alisema Mkurugenzi huyo.