NA MWANDISHI WETU
KATIKA maisha ni dhabi binadamu kukata tamaa kwa sababu hujiu wapi mafanikio yako yataanzia licha ya changamoto zitakazokukabili.
Kukata tamaa ni ishara ya kushindwa lakini wako waliofanikiwa baada ya kupiga moyo konde na kukabiliana na shida na dhiki na hatimae wameshinda.
Jamila Borafya Hamza (maarufu Choklat Colour) ni Mwenye ulemavu wa uoni mwenye miaka 23 ni mfano wa wasichana wenye ulemavu aliogombea nafasi ya uwakilishi Jimbo la Mwanakwerekwe katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Jamila licha ya ulemavu wake alionao hakukata tamaa kugombea nafasi hiyo kutokana na vikwazo mbalimbali alivyokumbana navyo wakati akijiandaa kugombea nafasi hiyo ikiwemo kukatishwa tamaa na baadhi ya wananchi.
Alisema wakati mchakato wa kugombea nafasi hiyo aliingia ulingoni na alikuwa Mwanamke pekee tena mwenye ulemavu aliogombea nafasi hiyo kati ya wanachama 12 waliojitokeza kugombea nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi.
Alieleza wapo waliomkatisha tamaa kutokana na ulemavu alionao na wapo waliomshauri aende akagombee nafasi ya viti maalum na kuacha kugombea uwakilishi Jimboni.
“Niligoma kugombea nafasi ya viti maalum niliwaambia hata kama nitashindwa katika mchakato wa kura za maoni lakini nitagombea Uwakilishi kwa sababu uwezo wangu ni kulitumikia jimbo na sio viti maalum”, alisema.
Alisema ndoto zake ni kuwa kiongozi wa jimbo kwa sababu, Wanawake wengi wanaogopa kwenda majimboni na ndio maana wengi wao wanang’ang’ania viti maalum na watu wenye ulemavu hugombea nafasi za viti maalum kupitia watu wenye ulemavu lakini yeye hakutaka kubebwa na kujiwezesha mwenyewe.
Jamila aliongeza kwa kusema “Safari yangu ya kuwa mwakilishi jimbo la Mwanakwerekwe iliishia katika mchakato wa kura za maoni na kukatisha ndoto zangu wajumbe walifanya ujumbe wao na sikubahatika kupata hata kura moja” alisema.
Alisema katika mchakato huo alijifunza mambo mengi ikiwemo kujiamini kwa sababu uwezo anao na bado hajakata tamaa na kusema kuwa ipo siku umuhimu wake utaonekana.
Alisema anaamini miongoni mwa sababu zilizomuangusha kutochaguliwa ni ulemavu wake alionao na kutokua na zawadi kwa ajili ya kuwapatia wajumbe.
“Wakati wa kuomba kura niliwaambia wajumbe kinachokwenda kuwatumikia katika baraza la Wawakilishi sio macho yangu wala ulemavu nilionao bali ni akili na maarifa na kuziwasilisha changamoto za wananchi”, alisema.
FEDHA KIKWAZO
Alisema fedha ni kikwazo kwa wanawake kugombea katika nafasi za uongozi kwa sababu uchaguzi ni gharama, hivyo wanawake wengi wenye kipato cha chini wanashindwa kugombea nafasi za uongozi licha ya kwamba wanawake wanaweza.
Jamila alianza harakati za kugombea nafasi za uongozi tokea akiwa Skuli ya msingi ambapo aliwahi kuwa Waziri wa habari Serikali ya wanafunzi Skuli ya Kiswandui, mwaka 2016 alishiriki katika Bunge la vijana na Mwenyekiti wa baraza la vijana wa shehia ya Mwanakwerekwe.
Alisema kukosa kwa nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, hakujadidimiza ndoto zake za kuwa kiongozi hivyo ataendelea kupambana na kumfikisha anapopataka ili kutimiza ndoto zake za kuwa kiongozi.
USHAURI

Jamila alishauri wanawake kushika nafasi nyingi za uongozi, jamii kuwaamini wanawake hasa Wenye ulemavu kuwa wanauwezo na wanamchango mkubwa kwa sababu wanaweza kujitolea, kupambana na kuleta mafanikio.
Aidha aliitaka Serikali kurekebisha sheria ambazo zitawapa fursa Wanawake hasa majimboni, vyama vya siasa kuweka vipengele maalum vinavyowapa nafasi Wanawake na watu wenye ulemavu.
“Kwa mfano katika Baraza la vijana katika sheria yake namba 16 ya mwaka 2013 inaweka wazi kwamba katika uchaguzi wowote kama kutakua na mtu mwenye ulemavu au mwanamke aliogombea hupewa kipaombele jambo ambalo halikupewa umuhimu”, alisema.
Aliwataka Wanawake waliopata nafasi za uongozi wasiwaangushe wanawake wezao kwa sababu watakapofanya vibaya wanawake wengine watakua hawaaminiki katika jamii lakini watakapo fanya vizuri watawaonesha njia nzuri na kufikia katika nafasi za uongozi.
Aliwataka wanawake wajitokeze kugombea nafasi za uongozi na wasikate tamaa kutokana na changamoto mbalimbali bali wapambane ili kuwa na wanawake wengi katika vyombo vya maamuzi.
Jamila ambae amezaliwa na ulemavu wa macho, amemaliza kidato cha nne mwaka juzi katika Skuli ya Sekondari Haile salasi Mjini Unguja lakini alishindwa kuendelea na masomo kutokana na matatizo ya afya.
Alisema atakapopata matibabu na afya yake itakapoimarika ataendelea na masomo ambapo lengo lake ni kusomea masuala ya elimu ya usimamizi na uongozi ili kutimiza ndoto zake.
Kati ya wawakilishi 50 wa Majimbo ya Uchaguzi ya Zanzibar waliomo katika Baraza la wawakilishi hakuna Mwakilishi mwenye ulemavu kutoka Jimboni licha ya kujitokeza kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu uliopita.