DOHA, Qatar
NAHODHA wa timu ya Taifa ya Ghana na mchezaji wa zamani wa Swasea City, Andre Ayew, amejiunga na matajiri wa Qatar, Al Sadd.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 alitarajia kutua Doha kukamilisha uhamisho wake ikiwa ni pamoja na kufanyiwa vipimo vya afya, kabla ya kumwaga wino unaoelezwa kuwa utakuwa ghali.

Inatajwa kuwa mchezaji huyo aliyekuwa sehemu ya kikosi cha Ghana kilichofika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia na kutolewa na Uruguay ya Luis Suarez atakuwa anapokea kiasi cha dola 200,000 kwa wiki.

Ayew atakuwa anafanya kazi chini ya kocha na mchezaji wa zamani wa Barcelona na Hispania, Xavi Hernandez ambaye sasa yuko Al Sadd.
Ayew alimalizia msimu wa 2020/2021 akiwa kama mfungaji bora wa michuano yote Swansea City akiwa na magoli 17 katika mechi 46.(Goal).