NA MWANDISHI WETU

MKURUGENZI wa ushirika wa AZE, Balozi Amina Sulum Ali, amesema taasisi hiyo imeamua kuwaunganisha wajasiriamali kwa lengo la kuzalisha bidhaa zenye viwango ili kukabiliana na ushindani wa biashara na kuwapatia masoko ya kuuza bidhaa wanazozalisha.

Balozi Amina alieleza hayo wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyowashirikisha wajasiriamali wanaounda ushirika huo, yaliyofanyika katika ukumbi wa Melinne Saccos, Mwanakwerekwe, Zanzibar.

Amefahamisha kuwa hatua hiyo itaondoa baadhi ya changamoto zinazowakabili wajasiriamali wadogo wadogo ikiwemo ya upatikanaji wa vifungashio na kuongeza mitaji ya kuendesha shughuli zao.

Alisema wajasiriamali wa Zanzibar wana uwezo wa kutengeneza bidhaa nzuri lakini baadhi yao hazina kiwango kinachokubalika hivyo uwepo wa ushirika huo utasaidia kuunganisha nguvu katika kutengeneza bidhaa zenye kukubalika na kutambulika duniani kote.

“Tatizo la wajasiriamali wetu sio ubunifu au uzalishaji bali ni ukosefu wa nyenzo za uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na mitaji ya kuwezesha huo uzalishaji,” alieleza Balozi Amina.

Kwa upande wake Afisa Ushirika kutoka Idara ya vyama vya ushirika Zanzibar, Faidha Hamran, alisema lengo la kuunganisha vikundi hivyo ni kutanua wigo na kuongeza nguvu ya uzalishaji wa bidhaa zenye viwango.

“Tunaamini katika ushirikiano huu, thamani ya bidhaa zinazozalishwa lakini pia kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazotosheleza mahitaji ya ndani na kusafirisha nje ya nchi,” alieleza Faidha.

Nao baadhi ya wajasiriamali waliohudhuria mafunzo hayo yaliyomalizika jana, walisema kuunganishwa kwa vikundi hivyo kutaleta mabadiliko katika utengenezaji wa bidhaa mbali mbali na kufikia malengo waliyojiwekea.

Ushirika wa AZE una vikundi 15 ambapo unatazamiwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbali mbali kwa kutumia malighafi zinazopatikana Zanzibar na ndio ushirika wa kwanza wa viwanda vya wajasiriamali kwa upande wa Zanzibar.