NA ASIA MWALIM

BARAZA la Mtihani la Tanzania limetoa matokeo ya mitihani ya kidato cha sita, ambapo ubora wa ufaulu umeimarika kutokana na idadi ya watahiniwa waliofaulu vizuri katika daraja la kwanza, la pili na tatu ambayo imeongezeka kwa asilimia 0.19.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani Taifa, Dk. Charles Msonde alieleza hayo huko katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi, alipokuwa akitangaza matokeo hayo.

Dk. Msonde alisema ongezeko hilo ni kutoka asilimia 97.74 kwenye matokeo ya mitihani ya mwaka 2020 ma kuwa asilimia 97.93 mwaka 2021 na kwamba ubora wa ufaulu wa wasichana umezidi kwa asilimi 0.10 ikilinganishwa na wavulana.

Alieleza kuwa Baraza la Mitihani Tanzania litafanya uchambuzi wa kina wa matokeo hayo kwa kila somo sambamba na kutoa machapisho ya uchambuzi huo yatakayo wasilishwa kwa wadau wa elimu zikiwemo skuli za sekondari za juu nchini kwa lengo la kuwawezesha walimu kutumia taarifa za uchambuzi katika kuongeza kiwango cha ufundishaji.

Alimtaja Percuy Astus Mussiba kutoka skuli ya Canossa ya jijini Dar es Salaam ndiye aliyeongoza mwanafunzi bora wa masomo ya sayansi mchipuo wa PCB, ambaye pia mwanafunzi huyo ameongoza orodha ya wanafunzi bora 10 wanawake.

Alimtaja Donald Rulers Mosile kutoka skuli ya Kisimiri Arusha kuwa ndiye mwanafunzi bora wa sayansi kwa wavulana akitokea mchipuo wa PCM.

Aidha alizitaja skuli 10 bora ni pamoja na Kisimiri, Kemebos, Dareda, Tabora Girls, Tabara Boys, Feza, Mwandet, Zakia Meghji, Kilosa na Mzumbe.

Aidha katibu huyo alisema Baraza hilo limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 22 wa skuli ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo, hivyo watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani wa kidatop cha sita Mei 2022 kama watahiniwa wa shule.

Akizungumzia matokeo ya mtihani yaliofutwa alisema Baraza ka Mtihani Tanzania limefuta matokeo yote ya watahiniwa 27 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani, ambao 25 ni watahiniwa wa skuli na wawili ni watahiniwa wa kujitegemea.

Hata hivyo baraza Baraza la Mitihani Tanzania limetoa pongezi kwa kamati za Uendeshaji Mitihani za Mkoa na Halmashauri/ Manispaa nchini, wakuu wa shule na wasimamizi wa mtihani uliofanyika Mei mwaka 2021 kwa kuzingatia na kusimamia taratibu za uendeshaji mitihani, hivyo kuzuia udanganyifu kufanyika.