NA KHAMISUU ABDALLAH

BEI ya mafuta ya taa, petroli na dizeli zimeendelea kuongezeka katika mwezi Julai kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya gharama za uingizaji wa bidhaa hiyo katika bandari ya Dar es Salam.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Mamlaka ya Udhitibi wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Khudhaimat Bakar Kheir, alitangaza bei hizo zitakazoanza leo, alisema bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imepanda ukilinganisha na mwezi uliopita.

Alisema katika mwezi huo, lita moja ya petroli itauzwa kwa shilingi 2,327 badala ya shilingi 2, 272 ya mwezi uliopita ikiwa ni ongezeko la shilingi 55 sawa na asilimia 2.42.

Khudhaimat alieleza kuwa mafuta ya dizeli yatauzwa kwa shilingi 2,222 kwa lita kutoka shilingi 2,182 katika mwezi uliopita ikiwa ni tofauti ya shilingi 40 sawa na asilimia 1.83.

Kwa upande wa mafuta ya taa, alisema bei ya rejareja itakuwa ni shilingi 1,608 kwa mwezi huu kutoka shilingi 1,546 iliyokuwa ikiuzwa mwezi uliopita tofauti ya shilingi 62 sawa na asilimia 4.01.

Alizitaja sababu zilizopelekea kupanda kwa bei hizo, alisema ni pamoja na kubadilika kwa wastani wa bei za uuzaji wa bidhaa hizo katika soko la dunia, thamani ya shilingi ya Tanzania kwa dola za kimarekani, gharama za usafiri, bima na ‘Premium’ hadi Zanzibar, kodi za serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Hata hivyo, alisema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani kwa mwezi uliopita ili kupata kianzio cha kufanyika mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi huu.

Sambamba na hayo, alibainisha kuwa licha ya kuwa mafuta yameongezeka lakini yapo ya kutosha kwa matumizi ya Zanzibar kwa mwezi mmoja.

Mbali na hayo alisisitiza kwamba ZURA haiamui kupanda na kushuka kwa bei hiyo bali inaangalia vigezo ambavyo vinafanywa kwa uwazi.

Hivyo, aliwaomba wananchi kuhakikisha kuwa bei zilizotangazwa ndio bei halali na kuwasisitiza kununua mafuta katika sheli zilizokuwepo kihalali ili kuepuka kuuziwa mafuta ya magendo na kudai risiti.