NA BENNY MWAIPAJA, ZANZIBAR
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kufanya tafiti mbalimbali zitakazosaidia kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia sekta za uchumi wa bluu pamoja na utalii.
Masauni ametoa maagizo hayo alipofanya ziara ya kikazi kwenye Tawi la Benki Kuu ya Tanzania lililoko kisiwani Unguja-Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kutembelea taasisi zilizochini ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Alisema kuwa Zanzibar inategemea uchumi wa bluu ikiwemo masuala ya uvuvi pamoja na sekta ya utalii kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake hivyo utafiti katika Nyanja hizo utasaidia kubaini njia bora za kuharakisha ukuaji wa uchumi wake kupitia Sekta hizo muhimu.
“Mazingira ya Uchumi wa Zanzibar ni tofauti na mazingira ya uchumi wa Bara, kuna maeneo ambayo katika uchumi wa Zanzibar yamepewa kipaumbele likiwemo suala la uchumi wa blue, na utalii, hivyo kuna kila sababu Benki Kuu ya Tanzania kufanya tafiti katika maeneo hayo ili kuishauri vyema Serikali”, alieleza Mhandisi Masauni.
Nae Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, aneyesimamia uthabiti wa sekta ya fedha pamoja na kusimamia Tawi la Benki Kuu-Zanzibar Dk. Bernard Kibesse, amemhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni kwamba maelekezo aliyoyatoa yatatekelezwa.
Alisema kuwa Benki hiyo tayari imeanza mchakato wa kufanya tafiti mbalimbali zitakazo saidia kukukuza na kuimarisha uchumi wa Zanzibar pamoja na kutekeleza sera za fedha kwa manufaa ya nchi hiyo na Taifa kwa ujumla.
“Tumesikiliza maagizo yako hasa ya kufanya tafiti kuhusu hali ya uchumi wa Zanzibar kwa kujikita zaidi katika uchumi wa Blue na utalii maeneo ambayo ndiyo nguzo kuu za uchumi wa Zanzibar”, alieleza Dk. Kibesse.
Naye Mkurugenzi wa BoT Tawi la Zanzibar Dk. Camillius Kombe, alieleza kuwa Sera imara za fedha zimeiwezesha Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuwa na uchumi imara pamoja utulivu wa mfumuko wa Bei ambao hivi sasa hauzidi asilimia moja.
Alisema kuwa kumekuwepo na utulivu wa bei visiwani Zanzibar kwa muda mrefu, ambao unatokana na Sera za Fedha kuwa na ufanisi kwa upande wa Zanzibar na imetokana na BoT Zanzibar kutoa hali halisi na mikakati ya kukuza uchumi na kuipeleka kwa watoa maamuzi.