GABORONE, BOTSWANA
BOTSWANA imefichua jiwe kubwa na jeupe la almasi lenye ukubwa wa karati 1,174, likiwa ndio jiwe la pili kwa ukubwa kuchimbuliwa nchini humo mwezi huu.
Almasi hiyo iligunduliwa Juni 12 na kampuni ya machimbo ya madini ya Canada- Lucara na kuwasilishwa kwenye hifadhi ya taifa ya madini iliyopo katika mji mkuu Gaborone.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo Naseem Lahri ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Almasi hiyo ni ya tatu kwa ukubwa duniani.
“Hii ni historia kwetu na kwa Botswana pia,” alisema Lahri.Mwezi uliopita, jiwe lililokuwa na uzito wa karati 1,098 -lilionyeshwa kwa Rais Mokgweetsi Masisi, baada ya kampuni ya almasi ya Debswana, kuligundua Juni mosi mwaka huu.
Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi aliushirikisha umma katika picha za pamoja na jiwe hilo la thamani.