‘NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza taasisi ya ‘Brenthurst Foundation’, kwa kufanikisha utafiti unaohusu utekelezaji wa mipango na sera za kiuchumi kwa maendeleo ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana ikulu jijini Zanzibar mara baada ya kupokea taarifa ya utafiti ambao utasaidia kufikiwa ufanisi katika kuinua uchumi wa Zanzibar.
Alisema lengo la taasisi hiyo kufanya utafiti ni kuweza kushirikiana vizuri na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala mbali mbali ya utungaji na utekelezaji wa mipango na sera za kiuchumi.
Alifahamisha kuwa kuna sababu za kuipongeza timu hiyo ambayo imefanya utafiti kwa kipindi kifupi ikiwa na lengo la kusaidia utekelezwaji wa mipango ya uchumi kwa haraka.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imejikita zaidi katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu kutokana na kujaaliwa kuwa na rasilimali ya bahari.
Alisisitiza kwamba pamoja na Zanzibar kuzungukwa na bahari lakini inaonekana kwamba bado rasilimali hiyo haijatumiwa ipasavyo katika suala la uchumi.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha sera ya uchumi wa buluu inaimarika kuna sekta muhimu ambazo zimepewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na sekta ya utalii, uvuvi, miundombinu na sekta ya mafuta na gesi asilia.
Dk. Mwinyi alieleza kuwa licha ya changamoto zilizokuwepo ikiwemo ya mtaji, lakini juhudi za makusudi zinachukuliwa na serikali huku akielezea kufarajika kujitokeza kwa taasisi zinazounga mkono juhudi hizo.
Alitumia fursa hiyo kumpongeza rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo na timu yake akiwemo waziri mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya “Brenthurst Foundation” Greg Mills pamoja na Jonathan Oppenheimer ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi hiyo.