NA MWANDISHI WETU, DODOMA

MWENYEKITI wa chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameeleza kuwa amepokea kwa mshituko na masikitiko kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa ccm mkoa wa kusini unguja, Ramadhan Abdalla Ali ‘Kichupa’, kilichotokea jana.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, idara ya Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ilieleza kuwa Samia ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifo hicho kimepoteza kiongozi mzalendo, mwenye msimamo na muumini wa kweli wa muungano, Mapinduzi na siasa za utaifa.

“Marehemu Mzee kichupa hakuwa tu kiongozi na mwanasiasa hodari bali pia alikuwa mwalimu, mwelekezi na mshauri mzuri wa masuala ya uongozi, uzalendo, utaifa, historia, utawala na uendeshaji wa masuala ya siasa,” alinukuliwa Rais Samia katika taarifa hiyo.

Aidha Shaka alieleza kuwa, Mwenyekiti huyo aliyezaliwa mwaka 1958 katika kijiji cha Jambiani, wilaya ya Kusini, Unguja, katika uhai wake ameshika nyadhifa mbali mbali ndani ya chama toka enzi za AFP, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika uhai wake, marehemu ‘Kichupa’ aliwahi kuwa Katibu wa CCM wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mbunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kusini Unguja nafasi aliyodumu nayo hadi kifo chake.

Marehemu Kichupa alizikwa jana alasiri kijijini kwao Jambiani Kibigija, wilaya ya kusini, mkoa wa Kusini Unguja, ambapo viongozi mbali mbali wa chama na serikali walihudhuria.