NA MADINA ISSA
MSIMAMIZI wa uchaguzi wa jimbo la Chwaka, Said Ramadhan Mgeni, amemtangaza Ali Hassan Mambo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Diwani mteule wa wadi ya Chwaka baada ya Haji Omar Iddi wa Chama cha ACT Wazalendo kujiondoa katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 14, mwaka huu.
Akitangaza uamuzi huo katika Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wilaya ya Kati Unguja, Said alisema umefanyika kwa mujibu wa kifungu 59 (b) cha sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.
Alieleza kuwa Haji amabae awali alichukua fomu kuomba uteuzi, kupeleka barua ya kujitoa katika mchakato wa uchaguzi juzi asubuhi kabla ya muda wa mwisho wa kurudisha fomu.
Alisema kutokana na hali hiyo tume inamtangaza mgombea pekee kuwa mshindi ili kuziba nafasi ya aliyekuwa diwani wa wadi hiyo Mlenge Khatib Mlenge, aliefariki dunia mapema mwaka huu.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo, Mambo, aliwashukuru viongozi na wanachama wa CCM, alisema kwa ushirikano walipompatia na kuahidi kushirikiana nao ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Sambamba na hayo, aliahidi kuendeleza msimamo waliokuwa nao viongozi wa CCM na kuwahimiza kuendelea kuwaunga mkono viongozi wa chama hicho, akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katibu wa chama hicho, mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Mzee Suleiman, alisema hatua hiyo inadhihirisha uimara wa chama hicho na kukubalika kwake kwa wananchi.