NA MWANDISHI WETU, DODOMA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha  kiongozi wa zamani wa chama cha soka nchini Said Hamad Elmamry na Mwanamuziki maarufu wa bendi ya Kilimanjaro (wana njenje) Waziri Ally Kisinger.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ilieleza kuwa Mwenyekiti wa chama hicho ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema vifo hivyo ni pigo kwa tasnia ya michezo, sheria pamoja na muziki.

“Tunaziombea familia za Mwanasheria Elmamry na Waziri Ally kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira na ustahamilivu,” alieleza Samia.

Mwanasheria Said Elmamry katika maisha na uhai wake aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM Tanzania  2009 – 2018, Mkuu  wa Polisi Mkoa Morogoro, Wakili mashuhuri, Mjumbe wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika Mashariki (CECAFA) na Mwenyekiti  wa Chama Cha Mpira wa Miguu (FAT) kwa miaka kadhaa.

Aidha taarifa hiyo ilimtaja mwanamuziki Waziri Ally Kisinger kuwa ameacha unyonge na simanzi katika anga la muziki kutokana na umahiri wake wa upigaji wa kinanda, ubunifu wa midundo, utunzi wa nyimbo na uimbaji wake.

“Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaziombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze Roho za marehemu mahali pema peponi pia  kinaziombea familia za marehemu hao azipe  ustahamilivu na uvumilivu katika kipindi hiki cha kuondokewa na wapendwa wao,” ilieleza taarifa ya Shaka.