NA TUWERA JUMA (MCC)

SHEHA wa Shehia ya Bububu Chemchem Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, Ame  Makame Ame, amewapongeza wananchi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kupokea chanjo ya maradhi ya kipindupindu, zoezi ambalo limemalizika jana likiwa katika hali ya utulivu.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Zanzibar Leo, katika kituo cha Hud hud Islamic nasari skuli, alisema wanachi wa shehiya hiyo wameupokea wito huo kwa kujitokeza kwa wingi kufanikisha suala hilo.

Alisema baadhi ya wanachi wamekuwa wakiitafsiri chanjo hiyo kwa maneno mabaya kwa kuisingizia inapunguza nguvu za kiume na kuwadhuru wanzanzibari, jambo  ambalo halina ukweli wowote ndani yake.

Alifahamisha wanachi wamejitokeza kwa wingi huku wanawake na watoto ila kwa upande wa wanaume na vijana hawana muamko mkubwa, hivyo aliwaomba kuja kwa wingi kwa sababu chanjo hiyo ni kwa ajili ya kijikinga na maradhi ya  mripuko.

“Wito wangu kwa wananchi ambao wanawafungia watoto ndani waache mara moja kwani serikali yetu haiwezi kutuletea sumu wananchi wake “,alisema Ame.

Nae mjumbe wa Sheha wa shehia hiyo kwa niaba ya wananchi,  Tausi Hassan, alisema kina mama wajitahidi kuwashajihisha  kina baba kwa ajili ya kuja kushiriki katika zoezi hili na wawapatie elimu kwa sababu wao ndio wanaojuwa tabia za waume zao kwani maradhi yanapokuja hayachagui.

Nae Mjumbe wa Sheha wa Shehia ya Mikarafuni Wilaya ya Magharibi ‘B’ Miraji Fadhil Abdala, amewataka wananchi  kuendelea kudumisha amani katika zoezi la chanjo ya kipindupindu .