NA BAHATI HABIBU, MAELEZO
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ambae pia ni mbunge wa jimbo la Uzini, Khamis Hamza Chilo, amewataka madaktari na wahudumu wa afya kutoa huduma bora licha ya mazingira magumu wanayokutana nayo.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada wa vifaa kwa ajili ya vituo mbalimbali vya afya, huko Mwera wilaya ya kati Unguja, mbunge huyo alisema jimbo la Uzini linahitaji mikakati madhubuti ili wananchi wa jimbo hilo waweze kupata huduma bora za afya.
Alisema madaktari na wahudumu wa afya bado wanakabiliwa na changamoto, ikiwemo uhaba wa vifaa, na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na Serikali, wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa jimbo hilo.
“Kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi na viongozi wa jimbo la Uzini kwa kushirikiana na serikali tutazitatua changamoto hizi kila hali itakaporuhusu”, alisema.
Alieleza kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na jitihada za kuhakikisha wananchi wote wa Zanzibar wanapatiwa huduma bora za afya nchini, hivyo aliwataka wahudumu wa afya kufanya kazi kwa bidii.
Alisema msaada huo wa magodoro na mito wenye thamani ya shilingi 2,275,000/= utatumika katika vituo vya afya ambavyo vinahudumia wazazi, akinamama na watoto.
Naye Mwakilishi wa jimbo hilo, Haji Shabani Waziri aliwataka wananchi kuchukua tahadhari ya maradhi ya corona ambayo tayari wizara ya afya ya Zanzibar imethibitisha kuwepo kwa wagonjwa wa corona Zanzibar.
Aidha aliwataka madaktari kutumia taaluma yao katika kutoa elimu kwa Jamii ili kujikinga na maambukizi ya corona, ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji na sabuni na vitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Naye ofisa tabibu wa kituo cha afya Mwera, Dokta Salum Makame ameushukuru uongozi wa jimbo la Uzini kwa Juhudi wanazozichukua za kuimarisha sekta ya afya katika Jimbo hilo.