BEIJING, CHINA
TRENI yenye uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilomita 600 kwa saa imezinduliwa katika eneo la Qingdao nchini China.
Treni hiyo ya mfumo wa Magliev iliotengenezwa na shirika la reli nchini China ndio treni yenye kasi zaidi duniani.
Aidha treni hiyo inaonekana kuelea angani kutokana na nguvu za umeme ambazo zinazoifanya kuonekana kuwa juu ya barabara ya reli.
Liang Jianying, naibu meneja na muhandisi mkuu wa shirika la CRRC Sifang , aliambia vyombo vya habari nchini humo kwamba mbali na kasi yake , treni hiyo haina kelele na inahitaji uangalizi mdogo ikilinganishwa na treni zengine zenye kasi ya juu
Inaelezwa kuwa reli yenye kasi ya juu nchini China ni kipaumbele , kukiwa na lengo la kuunganisha miji yake mikuu kwa treni ili kupunguza muda na gharama za usafiri ndani ya taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu duniani.
Hata hivyo kwa sasa , wastani wa kasi ya treni nchini humo ni kilomita 350 kwa saa , huku ndege zikiendeshwa katika kasi ya kati ya kilomita 800 hadi 900 kwa saa.
Kwa sasa China ina reli moja pekee ya mfumo wa Magliev inayotumika kibiashara, na inaunganisha uwanja wa ndege wa Pudong huko Shanghai na kituo cha barabara cha Longyang mjini humo.
Safari hiyo ya kilomita 30 huchukua takriban dakika saba na nusu huku treni hiyo ikisafiri kwa kasi ya kilomita 430 kwa saa moja.