KWA zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa tangu kuripotiwa ugonjwa wa corona, ugonjwa huo uliosambaa pembe zote za dunia umesababisha hasara kubwa duniani ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kwa pamoja baina ya shirika la biashara na maendeleo la Umoja wa Mataifa UNCTAD na shirika la Umoja wa Mataifa la utalii UNWTO, imebainisha kuwa corona imeathiri sana sekta ya utalii.

Kwa mujibu wa mashirika hayo athari za janga la corona katika sekta ya utalii inaweza kusababisha kupotea kwa zaidi ya dola trilioni 4 kwa uchumi wa dunia na hivyo nchi mbalimbali kuathirika.

Mwezi Julai mwaka jana, UNCTAD ilikadiria kuwa kusimama kwa utalii wa kimataifa kutagharimu uchumi wa dunia kati ya dola trilioni 1.2 na dola trilioni 3.3, huku hasa kwa mwaka huu itategema pakubwa fursa za upatikanaji wa chanjo ya ugonjwa huo.

“Dunia inahitaji juhudi za kimataifa za chanjo ambazo zitawalinda wafanyikazi, kupunguza athari mbaya za kijamii na kufanya maamuzi ya kimkakati kuhusu utalii, ikizingatia mabadiliko ya muundo”, amesema Isabelle Durant, kaimu katibu mkuu wa UNCTAD.

Naye katibu mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili aliongeza kuwa utalii ni njia ya maisha kwa mamilioni ya watu, na kuendeleza chanjo ili kulinda jamii na kusaidia kurejea kwa usalama katika utalii.

Alisema kuendeleza kutoa chanjo kwa ajili ya kuzilinda jamii na kuwezesha kuanzishwa tena shughuli za utalii ni muhimu kwa sababu kutachochea fursa za kupatikana ajira na uzalishaji wa rasilimali zinazohitajika.

Pololikashvili alisema katika taarifa yake kuwa utalii ni njia ya kuleta mapato kwa mamilioni ya watu ulimwenguni hivyo kuathirika kwa sekta hiyo kumeathiri maisha ya watu.

Ripoti hiyo imesema kusitishwa kwa safari ulimwenguni kote tangu mwanzo wa janga la corona kulisababisha hasara ya dola trilioni 2.4 katika sekta ya utalii na zile zinazohusiana na shughuli za utalii hapo mwaka jana.

Mashirika hayo yalibainisha kuwa hasara kama hiyo inaweza kutokea mwaka huu hasa kutokana na kusuasua kwa upatikanaji na usambazaji wa chanjo za kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Zuio la kusafiri lilisababisha kuongezeka kwa wastani wa asilimia 5.5 ya ukosefu wa ajira kwa watu wasio na ujuzi. Wakati huo huo wafanyakazi wa sekta ya utalii katika nchi ambazo hazina mfumo wa kuwalipa watu wasio na ajira wanatarajiwa kukosa kipato na hivyo kuwasababishia matatizo zaidi kutokana na kukosa fedha za kujikimu.

Watalii wa kimataifa wamepungua kwa karibu bilioni 1, au asilimia 73, mwaka 2020, wakati katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 kushuka kulikuwa karibu asilimia 88, imesema ripoti hiyo.

Nchi zinazoendelea zimebeba mzigo mkubwa wa athari za janga la COVID-19 kwenye utalii, huku kukikadiriwa kupungua kwa watalii wanaowasili kati ya asilimia 60 na asilimia 80.

Tatizo limekuwa kubwa zaidi hasa ikizingatiwa kuwa mataifa hayo yaanyoendelea ndiyo yanayokabiliwa na ukosefu mkubwa wa usawa wa chanjo.

Mashirika hayo yamesema kutolewa kwa mfumo wa chanjo ya COVID-19 kumeongeza pigo la kiuchumi kwa sekta ya utalii katika mataifa haya, kwani wangeweza kuchangia hadi asilimia 60 ya upotezaji wa pato la taifa.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi kukosa watalii kutokana na corona ni ya kaskazini mashariki mwa Asia, Asia ya Kusini, Oceania, Afrika Kaskazini na Asia ya kusini. Maeneo ya Amerika Kaskazini, Ulaya magharibi na Caribbean hayakuathirika sana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo sekta ya utalii inatarajiwa itakwamka haraka katika nchi zilizo na viwango vya juu vya chanjo ulimwenguni zikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Marekani.

Hata hivyo, watalii wa kimataifa hawatarudi katika viwango vya kabla ya janga hadi mwaka 2023 au baadaye, kwa sababu ya vizuizi kama vile vya kusafiri, kuzuia virusi kusambaa kwa kasi, imani duni ya wasafiri na mazingira duni ya kiuchumi.

Ripoti imebainisha kuwa kurejea kwa utalii kunatarajiwa kukua katika nusu ya pili ya mwaka huu, lakini kutakuwa na upotevu wa kati ya dola trilioni 1.7 na dola trilioni 2.4 mwaka huu wa 2021, kutokana na uigaji ambao unatenga mipango ya kuchochea utalii na sera kama hizo.

Msharika hayo yamesisitiza katika ripoti yao  juu ya utoaji wa chanjo kwa wote ili ulimwengu uweze kuifufua sekta ya utalii na kukuza uchumi katika nchi mbalimbali duniani.