NA  MADINA ISSA

KASI ya mfumko wa bei kwa mwaka uliomalizikia mwezi wa Juni 2021, imepanda na kufikia asilimia 1.9 ikilinganishwa na Mwezi wa Mei ambapo ulikuwa asilimia 0.8.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Khamis Abrahman Mshamu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mazizini mjini Unguja jana.

Alisema, mfumko wa bei wa chakula na vinywaji visivyokua na vileo umeshuka na kufikia asilimia 0.1 ikilinganishwa na asilimia 0.4 mwezi wa Mei.

Alisema mfumko wa bei wa chakula umefikia asilimia 0.2 ikilinganishwa na asilimia 0.4 kwa mwezi wa Mei ambapo faharisi za bei kwa mwezi wa Juni 2021 zilikuwa 117.7 na Juni 2020 ilikuwa asilimia 117.5

Aidha, alisema, mfumko wa bei usio wa chakula umeongezeka kufikia asilimia 3.2 kwa mwezi Juni ambapo mwezi Mei ulikuwa 0.1 na kuongezeka kwa mfumko huo  kumepelekea kuongezeka kwa bei za bidhaa.

Alizitaja bidhaa hizo ni mchele wa mapembe (asilimia 7.0), unga wa ngano (asilimia 9.6), samaki (asilimia 7.7), mafuta ya taa (asilimia 33.0), petroli (asilimia 42.2) na dizeli (asilimia 28.7).

Hata hivyo, alisema, mfumko wa bei wa mwezi kwa faharisi ya Juni mwaka 2021 umefikia asilimia 0.3 ukilinganishwa na asilimia 1.1 ya mwezi wa Mei ambapo mfumko wa bei wa bidhaa za chakula na vinywaji visivyo na vileo umefikia asilimia 1.7 ikilinganishwa na 2.2 mwezi wa Mei.

Alisema kushuka kwa mfumko wa bei wa mwezi kumepelekea kushuka kwa bidhaa kama unga wa ngano (asilimia 0.7), samaki (asilimia 0.2), ndizi za mtwike (asilimia 11.8) na sukari (asilimia 1.1).

Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Estella Ng’oma, alisema, sababu za kuongezeka mfumko wa bei kulichangiwa na baadhi ya bidhaa kupanda bei yakiwemo mafuta ya petroli na dizeli na kupelekea vitu vyengine kupanda bei.