NA ZAINAB ATUPAE

MKUU wa wilaya ya Kusini Unguja, Rashid Makame Shamsi, amewataka walimu wa skuli ya Dalailul-Khaiurat, kuendeleza jitihada zao ili kuwapatia elimu bora wanafunzi wao itakayo wasaidia  katika maisha yao ya duniani na kesho akhera.

Mkuu huyo alisema hayo alipokuwa akizungumza katika ufunguzi wa Mabaara ya Sayansi, kuwapongeza wanafunzi waliofanya mitihani ya taifa 2020 na kusherehekea kwa kutimia miaka 10 tangu kuanzishwa kwa skuli hiyo.

“Utoaji wa elimu wenu ni nzuri ambao unahitaji kupigiwa mfano kwa skuli zote za Mkoa wetu mumetunawisha uso kwani wilaya yetu kwa masuala ya elimu tukonyuma hasa katika matokeo ya kitaifa”,alisema.

Aidha aliwataka walimu hao kujitolea na kuwafundisha walimu wa skuli za serikali masuala ya nidhamu na uwajibika kwani walimu wa skuli za serikali kwa upande wa kusini wako nyuma katika masuala ya uwajibikaji.

Sambamba na hayo aliwataka walimu hao kuitumia ipaswavyo maabara hiyo kwa kutoa wanafunzi bora watakao kuwa mfano kwa wengine.

“Maabara hii ni nzuri tunataka iwe mfano kwa wengine kwa kutoa wanafunzi bora ambao watakuwa watendaji kazi katika nchi yao,”alisema.