ACCRA, Ghana
NAHODHA wa Black Stars, Andre Dede Ayew, amesherehekea baada ya kuibuka kama Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Ghana.

Ayew alitawazwa kama mwanasoka bora katika toleo la tatu la Tuzo za Soka za Ghana ambazo zilifanyika wiki iliyopita.

Picha iliyoonekana kwenye ukurasa wake wa Instagram inaonyesha nahodha huyo wa Black Stars akitoa hotuba yake baada ya kupokea tuzo yake.
Alikuwa amezungukwa na kaka yake mkubwa, Rahim Ayew, na Waziri wa Vijana na Michezo, Mustapha Ussif.

Akishiriki picha hiyo, Dede Ayew aliwashukuru Waghana kwa kumuunga mkono kila wakati. Alionyesha shukrani kwa heshima aliyofanyiwa. Dede pia aliwapongeza wateule wengine kwenye usiku huo akisema wote walikuwa washindi.

“Ahsanteni watu wa Ghana kwa msaada wenu mzuri kila wakati. Ninashukuru kwa heshima kama Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Ghana na ninashiriki utukufu huu na nyote. Hongera kwa wateule wote, sisi sote ni washindi! Mungu awabaraki”, ilisomeka kwenye picha hiyo.(Goal).