NA MARYAM HASSAN

DEREVA aliyedaiwa kumgonga mpanda baiskeli Leonad Juma Malaika na kumsababishia maumivu makali yaliyopelekea kifo chake, amepamdishwa katika kizimba cha mahakama ya mkoa Vuga kujibu tuhuma hizo.

Dereva huyo ni Khashil Suwes Juma (25) mkaazi wa Gongoni, alipanda kizimbani hapo mbele Hakimu wa mahakama ya mkoa Vuga Hussein Makame, ambapo Mwendesha Mashitaka, Mohammed Abdalla, alimsomea shitaka hilo mbele ya mahakama hiyo.

Mohammed, ambae ni Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alidai mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuendesha chombo cha moto bila ya hadhari na uangalifu na kusababisha kifo.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Disemba 29 mwaka jana majira ya saa 7:00 za mchana, huko Chuini njia ya Mawimbini wilaya ya Magharibi A’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo akiwa ni dereva wa gari yenye nambari za usajili Z696 DJ, akiwa anatokea Kwanyanya kuelekea Mfenesini, alipofika maeneo hayo aliendesha kwa uzembe na kumgonga mpanda baiskeli huyo.

Alieleza kuwa, mpanda baskeli huyo alipata majeraha usoni na kuvunjika mkono wa kulia, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa baada ya kusomewa kosa lake alikataa, huku upande wa mashitaka ukieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba mahakama kuahirishwa shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.

Hakimu Hussein, alimtaka  huyo kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya shilingi 500,000 na mshitakiwa asaini kima hicho hicho cha fedha.

Wadhamini hao pia walitakiwa wawasilishe kopi za kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi na barua za Sheha, huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Julai 27 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Mshitakiwa baada ya kupewa masharti hayo ametekeleza na yupo nje kwa dhamana.